Umoja wa Mataifa wataka kukomeshwa mzingiro wa Gaza
Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena umetoa wito wa kufutwa mzingiro wa eneo la Ukanda wa Gaza na kupelekwa misaada kwa wakazi wa eneo hilo.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric amesema kuwa umoja huo utaendelea kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya Wapalestina katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na Israel na kutafuta suluhisho la muda mrefu ikiwa ni pamoja na kukomesha mzingiro wa Gaza.
Dujarric amesema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuendelea kuwasaidia Wapalestina kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya kimsingi hadi kutakapopatikana suluhisho la kisiasa la kadhia ya Palestina.
Wakati huo huo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu, Ursula Mueller ambaye karibuni alitembelea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, ametoa wito wa kufutwa haraka mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Israel imekuwa ikiwashambulia wakazi wa Ukanda wa Gaza mara kwa mara kwa kutumia visingizio visivyo na msingi. Eneo hilo linazingirwa na utawala huo haramu kutokea angani, nchi kavu na baharini tangu mwaka 2006 na wakazi wake wanakabiliwa na mashaka na matatizo makubwa kwa ajili ya kupata huduma muhimu kama dawa, maji na chakula.