Velayati: Iran itaendelea kuunga mkono watu wa Palestina
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amepongeza mafanikio ya hivi karibuni ya harakati za kupigania ukombozi wa Palestina na kuongeza kuwa Iran itaendelea kuunga mkono watu wa Palestina.
Dkt. Ali Akbar Velayati ameyasema hayo Jumapili katika mazungumzo ya simu na Ismail Haniya, kiongozi wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, mwenye makao yake katika Ukanda wa Gaza.
Velayati amemfahamisha Haniya kuwa: “Tunafuatilia ushindi na mafanikio yako makubwa na kile unachofanya ni fahari kwa harakati ya kukabiliana na Israel.” Aidha Velayati amemfahamisha Haniya kuwa: “Wewe ni kigezo cha kuigwa katika ulimwengu wa Waislamu.”
Kwa upande wake, Haniya ameipongeza Iran kwa kuwa kituo cha kistratijia cha kuwaunga mkono Wapalestina na harakati zao za ukombozi.
Haniya ameendelea kusema kuwa, Wapalestina na harakati zao za mapambano ziko katika hali nzuri na wataendelea kuuhami Msikiti wa Al Aqsa unaokabiliwa na hujuma za utawala haramu wa Israel.
Mazungumzo hayo yamekuja huku utawala haramu wa Israel ukiwa umeshadidisha hujuma na ugaidi wake dhidi ya Wapalestina na maeneo matakatifu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hasa Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds au Jerusalem.
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni mapema Ijumaa Alfajiri walitekeleza hujuma dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ambapo waliwashambulia waumini waliokuwa wakitekeleza ibada katika msikiti huo katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Katika hujuma hiyo, zaidi ya waumini 160 walijeruhiwa na wengine 400 walikamatwa na askari hao vamizi wa Israel. Uchokozi huo umelaaniwa vikali kimataifa na pia katika nchi za Kiislamu na Kiarabu.