Mgogoro wa chakula nchini Afghanistan, sababu na wasababishaji
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekadiria idadi ya Waafghanistan ambao wanakosa chakula cha kutosha kuwa karibu milioni kumi na tano na kusisitiza haja ya kuendelea kutolewa msaada wa chakula kwa watu wasio na uwezo wa nchi hiyo.
Hii ni pamoja na ukweli kwamba wakati wa kukaliwa kwa mabavu Afghanistan mwaka 2001, Marekani iliahidi kutatua matatizo yote ya nchi hiyo. Lakini baada ya miongo miwili ya kuikalia kwa mabavu, Wamarekani walitoroka kwa madhila Afghanistan na sasa ulimwengu unashuhudia nchi isiyo na utulivu wala usalama sambamba na uhaba mkubwa wa chakula.
Hivi sasa mashirika ya kimataifa hayana uwezo wa kutoa mahitaji ya kimsingi kwa watu wa Afghanistan na hivyo kuna mgogoro mkubwa katika nchi hiyo.
Baada ya miongo miwili ya kukaliwa kwa mabavu sambamba na Marekani kuwadhalilisha watu Afghanistan, kile ambacho watu waliodhulumiwa wa nchi hiyo wamekirithi kwa Marekani ni matatizo yanayoongezeka, hasa njaa kali.
"Molvi Mofleh", mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema hivi kuhusu nukta hii.
“Suala la njaa halitishii tu hali ya sasa ya watu wa Afghanistan, bali pia linahatarisha usalama na afya ya kizazi kijacho cha nchi hii. Kwa sababu njaa na utapiamlo vinawaweka watoto wa Afghanistan katika hali mbaya sana ya maisha, ambayo inaweza kutishia afya ya kizazi kijacho cha jamii ya Afghanistan.
Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba kwa mujibu wa tangazo la WFP licha ya msaada wa chakula uliotolewa kwa watu wa Afghanistan, watu milioni 15 katika nchi hii hawakupata chakula cha kutosha mwezi Mei. Kwa hivyo, WFP imesisitiza ulazima wa kuendelea kutoa msaada wa chakula kwa Afghanistan. Kulingana na takwimu zilizochapishwa na Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 29 nchini Afghanistan wanahitaji misaada ya kibinadamu. Wakati Afghanistan ina ardhi ya kilimo yenye rutuba na maji, swali ni kwamba, je, ni kwa nini nchi hii inakabiliwa na tatizo la chakula? Katika kujibu swali hili muhimu, inatupasa kusema kwamba katika miongo miwili ya kukaliwa kwa mabavu Afghanistan, Marekani na Uingereza zilizuia utekelezaji wa mpango mbadala wa kilimo badala ya mihadarati aina ya mpopi (opium) nchini Afghanistan, kwa sababu walifaidika kwa kuuza mihadarati kupitia njia za mawasiliano za kimataifa walizokuwa wanazidhibit. Hivyo katika kipindi cha miaka 20 iliyopita ardhi yenye rutuba ya Afghanistan imekuwa ikitumika kukuza mihadarati kwa maslahi ya Marekani na waitifaki wake ambao walifaidika sana na biashara hiyo haramu.
Ali Khazaei, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema:
"Wafanyabiashara na mafia wa madawa ya kulevya pamoja na madola vamizi, walizuia utekelezaji wa miradi ya kilimo nchini Afghanistan katika miongo miwili iliyopita. Ardhi zilizotumika katika kilimo cha mihadarati zingeweza kutumika kukidhi mahitaji ya kimsingi ya chakula kwa watu wa Afghanistan. Katika historia ya Afghanistan, nchi hii haijawahi kutegemea sana misaada ya chakula ya kimataifa ili kuokoa maisha ya watu wake."
Kwa vyo vyote vile, Marekani inaendelea kuiwekea Afghanistan vikwazo na hivyo kuongeza kila siku matatizo ya watu wa nchi hiyo.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, lengo kuu la Marekani la kutoa mashinikizo ya ziada kwa watu wa Afghanistan ni kuanzisha utengano wa dini na siasa ili iweze kuhakikisha kuwa kizazi kijacho cha nchi hiyo kinafuata utamaduni potovu wa Kimagharibi.
Kwa hivyo, inaonekana kwamba kuundwa serikali imara nchini Afghanistan na kuimarisha umoja wa kitaifa na kuibua harakati kubwa katika sekta ya kilimo na viwanda ndio njia pekee ya kuinasua Afghanistan kutoka katika hali ya sasa. Hatua hizo muafaka zikichukuliwa bila shaka Marekani haitapata kisingizio cha kuendelea kuishinikiza nchi hiyo. Vinginevyo, Afghanistan itaendelea kuwa katika hatihati ya janga la kitaifa, na bila shaka, Taliban, serikali inayotawala nchi hii, ina jukumu zito la kusambaza chakula na huduma za afya kwa watu wa Afghanistan.