Kuendelea kugunduliwa makaburi ya halaiki ya watoto asili wa Canada
Katika miaka ya hivi karibuni, kugunduliwa makaburi ya halaiki na miili ya mamia ya watoto wenyeji waliozikwa kwa siri nchini Canada kumefichua mauaji ya kutisha na ubaguzi wa rangi uliofanywa dhidi ya wenyeji wa nchi hiyo, suala ambalo limewashangaza wanaharakati wengi wa kutetea haki za kiraia, viongozi wa kisiasa na wawakilishi wa maoni ya umma ndani na nje ya mipaka ya Canada.
Ugunduzi wa makaburi hayo ungali unaendelea kiasi kwamba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zaidi ya makaburi 1,300 ya watoto yamegunduliwa karibu na baadhi ya taasisi za kielimu za makanisa ambazo zilikuwa sehemu ya mfumo wa elimu kwa ajili ya watoto wenyeji wa nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, siku ya Jumatano moja ya makabila ya wachache ya wazawa asilia wa Canada yanayoishi magharibi mwa nchi hiyo lilitangaza kugunduliwa kwa kaburi la umati la watoto wapatao mia moja katika eneo hilo.
Kabila hilo la The English River First Nation limesema kwamba kilichogunduliwa kinahuzunisha sana. Kufikia sasa, makaburi 93 ambayo hayana alama yoyote yakiwemo ya watoto 79 na watoto wachanga 14 yamegunduliwa katika nchi hiyo.
Makaburi mapya yamegunduliwa kufuatia utafiti uliofanywa karibu na shule ya bweni ya wenyeji asilia inayoitwa Beauval katika eneo la Saskatchewan, Canada. Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Regina, majengo ya shule hiyo yaliharibiwa na wakaazi baada ya kufungwa mnamo 1995.
Kuanzishwa kwa shule za bweni kwa ajili ya wazawa asilia wa Canada imekuwa sehemu ya siasa za nchi hiyo za kufutilia mbali utambulisho wa wazawa hao na kisha kuchukua ardhi zao. Kwa mujibu wa nyaraka zilizochapishwa, kuanzia mwishoni mwa karne ya 19 hadi katikati ya muongo wa 1990, siasa hizo zilifuatiliwa kwa karibu sana na serikali ya Canada, ambapo kuanzishwa shule za bweni ilikuwa mojawapo ya mipango ya kufutilia mbali uwepo wa watoto wa Wahindi Wekundu katika nchi hiyo. Taasisi hizo za elimu zilikuwa zikiendeshwa kwa pamoja na Kanisa Katoliki na serikali ya Canada kwa lengo la "kuua fikra za wazawa asilia katika kipindi cha utotoni."
Walikuwa wakiwachukua watoto wa asili, kwa nguvu au kwa ahadi bandia za kuwaletea maendeleo, kutoka kwa familia zao na kisha kuwaweka kwenye shule za bweni. Wakiwa huko, watoto hao si tu walilazimishwa kusahau kugha na utamaduni wao, bali wengi wao walinyanyaswa kingono, kihisia na kimwili pia. Wengi wao walikufa kwa njaa, kazi ya kulazimishwa na unyanyasaji wa kimwili na kuzikwa kimya kimya katika makaburi ya halaiki bila familia zao kufahamishwa lolote kuhusu mauaji hayo.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kufichuliwa kwa ukubwa wa jinai hiyo kumepelekea viongozi wa serikali ya Canada, akiwemo Waziri Mkuu Justin Trudeau, kuyataja mauaji hayo kuwa maafa ya kihistoria yaliyotendwa na waliotangulia. Lakini hali halisi ya kijamii ya Canada inaonyesha kwamba mauaji ya kimbari ya wazawa asilia wa nchi hiyo yangali yanaendelezwa kwa mbinu mpya za kisasa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika miaka ya hivi karibuni, wanawake wa asilia wa Canada bado wana uwezekano wa kufa au kutoweka mara 12 zaidi kuliko wanawake wa jamii nyingine.
Marion Buller, msimamizi wa utafiti huo anasema kwamba licha ya hali na mazingira tofauti lakini wote waliotoweka na kuuliwa wana hali sawa ya kutengwa kiuchumi, kijamii na kisiasa, na walikabiliwa na ubaguzi wa rangi na wanawake wao kudhulumiwa kimpangilio katika jamii ya Kanada.
Suala hilo hupelekea wengi wao kuamua kujitoa uhai. Takwimu zinaonyesha kuwa kuna wanawake 35 wanaojiua kwa kila wanawake wa asili laki moja, wakati kiwango hicho ni tano kwa kila wanawake laki moja katika jamii ya wanawake wasio wa asili.
Ukweli wa mambo ni kwamba jinai na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa dhidi ya wenyeji wa Canada hayahusiani tu na siku za nyuma na historia ya nchi hiyo, bali ni jambo linaloendelea na kuacha nyuma madhara makubwa kwa jamii ya wakazi asilia wa nchi hiyo, licha ya kauli mbiu na madai ya uongo yanayotolewa mara kwa mara na serikali ya nchi hiyo kuwa inaheshimu na kutetea usawa na uhuru kati ya raia wote wa nchi hiyo.