Daesh imehusika na mlipuko wa Pul-e-Khumri nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i103468-daesh_imehusika_na_mlipuko_wa_pul_e_khumri_nchini_afghanistan
Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na mlipuko katika msikiti wa Imam Zaman (A.S) huko Pul--Khumri makao makuu ya jimbo la Baghlan kaskazini mwa Afghanistan. Watu wasiopungua 30 wameuawa shahidi na wengine 50 kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2023 08:59 UTC
  • Daesh imehusika na mlipuko wa Pul-e-Khumri nchini Afghanistan

Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na mlipuko katika msikiti wa Imam Zaman (A.S) huko Pul--Khumri makao makuu ya jimbo la Baghlan kaskazini mwa Afghanistan. Watu wasiopungua 30 wameuawa shahidi na wengine 50 kujeruhiwa.

Kundi la kigaidi la Daesh katika miezi ya karibuni limeshadidisha mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan khususan dhidi ya maeneo ya kidini ya Waislamu wa Kishia. Hata kama Taliban iliahidi kupambana vikali dhidi ya Daesh ili kuwadhaminia usalama wananchi wa Afghanistan, lakini kuendelea mashambulizi ya kigaidi ya kundi hilo nchini humo kunaonyesha namna Taliban ilivyoshindwa kutekeleza ahadi zake katika uwanja huo. Nukta nyingine ya kuzingatia ni hii kuwa kundi la Taliban linaoongoza huko Afghanistan linaamini kuwa Daesh haina uwezo wa kutekeleza oparesheni kubwa huko Afghanistan. Iwapo madai haya ya Taliban yatazingatiwa tunapasa kusema kuwa makundi mengine ya kigaidi pia yanaendesha hujuma nchini humo; ambapo kwa kustafidi na taswira ya Daesh yanajaribu kuibua hitilafu na kuzusha vita vya kidini huko Afghanistan.

Magaidi wa Daesh nchini Afghanistan 

Akram Arifi mchambuzi wa masuala ya kisiasa anazungumzia hili akisema: Katika kipindi cha zaidi ya miongo minne iliyopita mapigano ya Afghanistan hayajawahi kuwa ya kimadhehebu bali zaidi yamekuwa ni ya kikabila na ya kuwania madaraka. Kwa msingi huo, jitihada za kuibua vita vya kidini na hitilafu huko Afghanistan ni kadhia kutoka nje ambayo imekusudiwa kuchochea vita vya kidini nchini humo. 

Uongozi wa kundi la Taliban 

Ukweli wa mambo ni kuwa wananchi wa Afghanistan siku zote wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani na maelewano, na suala la vita vya kikabila na kisiasa pia ni kadhia waliyotwishwa wananchi hao na baadhi ya mirengo yenye kupenda kujitanua. Ni dhahir shahir kuwa wananchi wa Afghanistan wamedhihirisha kivitendo kuwa ni watu wanaopenda amani na urafiki; na kwa hakika hakuna kundi la kigaidi litakalokuwa na fursa ya kutoa pigo kwa usalama wa Afghanistan iwapo baadhi ya mirengo pia itaachana na utengano wa kisiasa na ukabila na badala yake isaidie mshikamo wa kitaifa kwa kuimarisha umoja wa kisiasa nchini humo. 

Aidha katika kalibu ya mchafukoge, watenda jinai wenye mfungamano na nchi ajinabi pia wanastafidi na hali hiyo ya mambo ili kufanikisha malengo yao ya kihalifu kwa sababu wao pia wanaendeleza maisha yao ya kihalifu kupitia kuendelea kutekeleza jinai mbalimbali huko Afghanistan. Assadullah Bashir mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Wananchi wa Afghanistan Shia au Suni wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani na maelewano; na kwa sababu hiyo jitihada za kuibua vita vya kikaumu na kimadhehebu nchini humo daima zimegonga mwamba. Pamoja na hayo, watenda jinai wanashambulia maeneo mbalimbali ya Waislamu wa Kishia ili kudhihirisha kuwa hawajakata tamaa katika njia hiyo, hata hivyo wananchi wa Afghanistan wameonyesha kivitendo hawataangukia katika mtego wa wahalifu hao, na watasambaratisha njama za magaidi kwa kudumisha mshikamano wa kitaifa na kidini kati yao. 

Ala kulli haal hakuna shaka kuwa kundi la Taliban linaloongoza Afghanistan linapasa kufanya juhudi za kuimarisha usalama wa taifa. Magaidi wamekuwa wakifuatilia kutekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya kidini, lakini kushindwa Taliban kuwalinda raia wanaokuwa katika maeneo ya ibada si jambo ambalo Taliban inaweza kulipuuza. Hii ni kwa sababu, kwa upande mmoja kushindwa Taliban kuyatokomeza makundi ya kigaidi huko Afghanistan kunaonyesha namna kundi hilo linavyotenda jinai kwa kutumia majina tofauti; na kwa upande wa pili, baadhi ya duru hazikanushi juu ya uwezekano wa kunufaika Taliban na hali ya mchafukoge huko Afghanistan. Hali hii ya mambo inapelekea kutiliwa shaka pakubwa utawala wa Taliban huko Afghanistan, na wakati huo huo inaipa Marekani kisingizio cha kuingilia tena masuala ya usalama ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.