Joe Biden: Mimi ni Mzayuni
Kwa mara nyingine tena rais wa Marekani amejigamba kuwa yeye ni Mzayuni na anaunga mkono jinai za Israel licha ya idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi hivi sasa kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza, kupindukia 30,000.
Kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Joe Biden, ambaye serikali yake inachangia kikamilifu jinai za Israel kwa njia mbalimbali zikiwemo za msaada kamili wa kijeshi, kifedha na kidiplomasia tangu jinai hizo zilipoanza tarehe 7 Oktoba 2023, dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, amejigamba kwenye mahojiano ya televisheni kwamba yeye ni Mzayuni na ataendelea kuunga mkono jinai hizo hadi pale HAMAS itakapofutwa kabisa.
Amesema kwa majivuno kwamba: "Ili kuwa Mzayuni, si lazima uwe Myahudi. Mimi ni Mzayuni. Lau kama Israel isingelikuwepo, hivi sasa asingekuwepo Myahudi yeyote duniani."

Utawala wa kibeberu wa Marekani ulitangaza mshikamano wake na utawala wa Kizayuni mara baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
Katika siku za mwishoni mwa mwezi Disemba 2023 pia, Biden aliwakaribisha Mayahudi katika Ikulu ya White House na kusema: Marekani itaendelea kutuma misaada ya kijeshi kwa Israel.
Pia amesema: Wakati miaka michache iliyopita niliposema kuwa si lazima kuwa Myahudi ili uwe Mzayuni, nilishutumiwa sana, lakini mimi ni Mzayuni. Tukiweka kando tofauti zetu na Waziri Mkuu wa Israel, niseme ukweli, ahadi yangu ya kuweko dola la Kiyahudi haiyumbi"
Dunia nzima inaendelea kulaani jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, lakini rais wa Marekani anaona fakhari kutangaza hadharani kuwa anaunga mkono kikamilifu jinai hizo.