Apr 30, 2024 03:51 UTC

Mtu mwenye msimamo mikali nchini Sweden amekivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa kuchoma moto nakala ya kitabu hicho.

Kituo cha runinga cha Russia Today kimechapisha picha za mwanamke akichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu huko Stockholm, mji mkuu wa Sweden. Russia Today imeripoti kuwa, mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Jade Sanberg, amefanya kitendo hicho kiovu akiwa amebeba msalaba mkononi.

Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zinamuonyesha mwanamke huyo aliyedai kuwa ni mwanahakati wa Kikristo akipewa ulinzi kamili na polisi ya Sweden iliyomruhusu kufanya kitendo hicho kinachochea chuki za kidini na kuvunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu zaidi ya bilioni mbili kote dunia kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza. 

Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Sweden kuruhusu vitendo viovu vya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu. 

Tangu 2023, wakati Rasmus Paludan, mwanasiasa wa Denmark wa mrengo wa kulia mwenye uraia wa Uswidi, alipochoma Qur'ani mbele ya ubalozi wa Uturuki nchini Sweden, vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara nchini humo.

Awali, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alilaani wimbi la vitendo vya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Volker Turk, alitangaza msimamo huo wa Umoja wa Mataifa katika mkutano wa ngazi ya juu wa kumbukumbu ya miaka 75 ya Tangazo la Haki za Binadamu Ulimwenguni na kuongeza kuwa, vitendo hivyo vya kuchukiza vya kuchoma moto nakala za Qur'ani vinalenga kuzusha mizozo baina ya jamii na nchi tofauti duniani.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa serikali na tawala za nchi za Ulaya kuchukua msimamo mkali dhidi ya vitendo hivyo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.