Colombia yakata uhusiano na utawala wa Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia ametangaza kukatwa uhusiano wa kidiplomasia wa nchi yake na utawala wa Kizayuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia Luis Murillo alisema siku ya Jumapili kwamba nchi yake chini ya uongozi wa Rais Costavo Pietro, imevunja uhusiano wake na utawala wa Kizayuni kutokana na utawala huo kutofuata sheria za kimataifa za kibinadamu kwa kuendeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Katika mahojiano na kanali ya Al Jazeera Murillo amesisitiza kuwa Colombia inaendelea kutekeleza uamuzi wa Rais wa nchi hiyo wa kufungua ubalozi wa Colombia huko Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia ameongeza kuwa Rais Costavo Pietro amekuwa na misimamo ya wazi tangu mwanzo ambapo amelaani vikali mauaji ya umati yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia amedokeza kwamba kwa muda sasa nchi yake imekuwa ikifanya juhudi za kuachiliwa huru mateka na kusitishwa mapigano lakini kuwa mauaji ya halaiki ya sasa hayavumiliki kabisa.
Huku akilaani mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni na kutaka yasitishwe mara moja, Luis Murillo ametoa wito wa kufanyika kongamano la kimataifa ili kufikia amani ya kusitishwa mauaji ya kimbari huko Gaza.
Tangu tarehe 7, Oktoba 2023 mwaka jana utawala wa mkibaguzi wa Israel umekuwa ukifanya mauaji kimbari katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi na hasa Marekani na kimya cha jamii ya kimataifa.
Tasisi za kutetea haki za binadamu zinasema jinai za utawala ghasibu wa Israel zimepelekea kuendelezwa mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina wanaouawa kinyama na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, tangu kuanza mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza wasio na ulinzi takriban watu elfu 36,000 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine elfu 80,400 wamejeruhiwa.