Mwanamke Mfaransa ahukumiwa miaka 3 jela kwa kuiunga mkono Palestina
(last modified Wed, 06 Nov 2024 02:23:50 GMT )
Nov 06, 2024 02:23 UTC
  • Mwanamke Mfaransa ahukumiwa miaka 3 jela kwa kuiunga mkono Palestina

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa mwanamke mmoja raia wa Ufaransa amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuliunga mkono na kulitetea taifa la Palestina linaloendelea kukabiliwa na mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel.

Idara ya Mahakama ya Ufaransa imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela mwanaharakati anayeiunga mkono Palestina kwa kuchapisha jumbe kwenye mitandao ya kijamii yenye kuliunga mkono taifa la Palestina na kulaani mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 

Hukumu hii ilitolewa jana katika mji wa Nice nchini Ufaransa dhidi ya mwanamama huyo aliye na umri wa miaka 34.

France Press imetangaza kuwa mwanamke huyo ni mama, muuguzi msaidizi na mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo cha mafunzo ya uuguzi ambaye amekuwa kizuizini tangu Septemba 19.

Mwanaharakati huyo muungaji mkono wa Palestina pia ameshiriki katika kuasisiwa Jumuiya kwa jina la " From Nice to Gaza" na alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa maandamano ya kuitetea Palestina katika mji wa Nice nchini Ufaransa.  

Mwanaharakati huyo alisema wakati wa kusilikilizwa kesi hiyo na wakati akijitetea kwamba: Kumetekelezwa mauaji ya kimbari  ambapo watu zaidi ya elfu 43 wameuawa na zaidi ya  laki moja kujeruhiwa.

Israel inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza 

Jamii ya kimataifa khususan jumuiya za kutetea haki za binadamu zimeendelea kulaani mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Gaza ambayo hadi sasa yameuwa karibu Wapalestina elfu 50.