Serikali ya Ujerumani yasambaratika
(last modified Thu, 07 Nov 2024 09:28:45 GMT )
Nov 07, 2024 09:28 UTC
  • Serikali ya Ujerumani yasambaratika

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amemfuta kazi waziri wa fedha na hivyo kuisambaratisha serikali ya muungano wa vyama ya nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.

Kwa mujibu wa Reuters, inatarajiwa kuwa, Scholz ataendelea kuongoza serikali ya wachache inayoshirikisha vyama vya Social Democrat na vyama vya mrengo wa Kijani, baada ya kumfuta kazi waziri wa fedha, Christian Lindner kutoka chama cha Free Democtratic.

Kwa upande wake shirika la habari la AFP limemnukuu kansela wa Ujerumani akiwaambia waandishi wa habari kuwa, Lindner amemvunja moyo sana katika masuala mengi. Haiwezekani kufanya kazi za maana serikalini kwa kuendelea kuwemo humo Lindner. 

Amesema yeyote aliyemo serikalini lazima atekeleze wajibu wake kama inavyotakiwa. Inabidi mtu abebe majukumu yake asikwepe.

Hivi sasa Olaf Scholz atalazimika kurudi tena bungeni kupigiwa kura serikali yake. Kama atakosa kura zinazotakiwa, itabidi kuitishwa uchaguzi wa kabla ya wakati wake. Iwapo kansela huyo wa Ujerumani atakosa imani ya bunge, itabidi uchaguzi wa haraka uitishwe mwishoni mwa mwezi Machi mwakani.

Jumatatu wiki hii, Robert Habeck, naibu wa Scholz alionya kuhusu kusambaratika serikali ya nchi hiyo akigusia mivutano mikali iliyomo ndani ya vyama vinavyounda serikali inayoongozwa na kansela Olaf Scholz.

Chama cha Social Democrat ambacho ni chama muhimu katika serikali ya muuungano ya Ujerumani, kinaunga mkono kuongezwa mishahara, marupurupu, bima na misaada ya kijamii. Lakini vyama vya mrengo wa kijani vinasema kuwa mambo ya kupewa kipaumbele na serikali ni masuala ya tabianchi na kulindwa mazingira huku chama kingine cha Free Democrat kikitaka zipewe kipaumbele siasa za kuongeza ajira na kuimarisha uchumi.