Australia nayo kuitambua rasmi Palestina katika mkutano ujao wa UNGA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129422-australia_nayo_kuitambua_rasmi_palestina_katika_mkutano_ujao_wa_unga
Serikali ya Australia nayo imetangaza kuwa, inatarajia kuitambua rasmi Palestina mwezi ujao wa Septemba.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 11, 2025 23:06 UTC
  • Anthony Albanese, Waziri Mkuu wa Australia
    Anthony Albanese, Waziri Mkuu wa Australia

Serikali ya Australia nayo imetangaza kuwa, inatarajia kuitambua rasmi Palestina mwezi ujao wa Septemba.

Waziri Mkuu wa Australia ametangaza kuwa, Canberra italitambua taifa la Palestina kwenye mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Septemba. "Canberra itatambua haki ya watu wa Palestina kuwa na nchi yao wenyewe," Anthony Albanese aliwaambia waandishi wa habari, kulingana na tovuti ya gazeti la Ufaransa la Le Figaro.

Le Figaro linasisitiza katika ripoti yake kwamba, jumla ya robo tatu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanalitambua taifa la Palestina, na takriban nchi 10 zimejiunga na harakati hii tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza.

Le Figaro linakumbusha kwamba mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, Australia na nchi nyingine 14 za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa na Kanada, "zilitoa wito" kwa jamii ya kimataifa kutambua taifa la Palestina, kufuatia mkutano wa Mawaziri wa Umoja wa Mataifa kuhusu ufumbuzi wa mataifa mawili kwa mzozo wa Israel na Palestina.

Mwezi Desemba mwaka jana, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio linalotaka kuwepo kwa mazungumzo ya kuaminika kwa ajili ya mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati. Kisha uliamua kuitisha "mkutano wa ngazi ya juu wa kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa suluhisho la serikali mbili" huko New York mwezi Julai. Ufaransa na Saudi Arabia zilipewa jukumu la kuongoza mkutano huo.

Ufaransa inawaongoza washirika wake barani Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Uholanzi, na Ubelgiji, katika kushinikiza kutambuliwa kwa Palestina kwa pamoja wakati wa mkutano huo muhimu.