Amnesty International yataka kukomeshwa mauaji huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129468-amnesty_international_yataka_kukomeshwa_mauaji_huko_gaza
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kimataifa kukomesha mauaji katika Ukanda Gaza.
(last modified 2025-08-12T23:01:13+00:00 )
Aug 12, 2025 23:01 UTC
  • Amnesty International yataka kukomeshwa mauaji huko Gaza

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kimataifa kukomesha mauaji katika Ukanda Gaza.

Amnesty International imelaani mauaji ya makusudi ya waandishi wa habari yanayofanywa na Israel na kutaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu mauaji ya waandishi wa habari huko Gaza.

Shirika hilo lilisema kuwa ripota wa Al Jazeera Anas Al-Sharif na wenzake walikuwa macho na sauti za Gaza na kwa uhodari waliendelea kuandika habari kutoka Gaza licha ya njaa na uchovu.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesisitiza kuwa, uchunguzi huru na wa uwazi unapaswa kufanywa kuhusu mauaji ya waandishi wa habari wa Palestina kwa lengo la kupatikana haki na kutoa fidia kwa familia zao.

Wanajeshi wa Israel hivi majuzi waliwauwa wafanyakazi watano wa televisheni ya Al-Jazeera wakiwemo waandishi habari Anas al Sharif na Mohammed Qareqa pamoja na wapiga picha Ibrahim Zaher na Mohammed Nofal katika shambulio la kuvizia kwenye hema la wana habari nje ya uwanja wa Hospitali ya Al Shifa katika mji wa Gaza. 

Watu wengine wawili waliuawa katika shambulio hilo la kuvizia la Israel.

Muda mfupi kabla ya kuuawa, Al Sharif, mwandishi habari mtajika wa televisheni ya Al Jazeera ambaye alifanya kazi kubwa ya kuripoti matukio mbalimbali ya vita vya Israel kutokea kaskazini mwa Gaza, aliandika katika ukurasa wake wa X kwamba: Israel imeanzisha  mashambulizi makubwa ya anga kwa kutumia mabomu yanayojulikana kama "mikanda ya moto"  katika maeneo ya mashariki na kusini mwa mji wa Gaza.