New Zealand: Benjamin Netanyahu amerukwa na akili
-
Christopher Luxon Waziri Mkuu wa New Zealand
Christopher Luxon Waziri Mkuu wa New Zealand amesema Benjamin Netanyahu anaonekana amerukwa na akili.
Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani, Christopher Luxson amesema kinachoendelea Gaza "ni cha kutisha kabisa." "Nadhani Netanyahu amekwenda mbali sana, nadhani amerukwa na akili, na nadhani tunachokiona usiku wa leo kwenye shambulio la Gaza City hakikubaliki kabisa."
Matamshi ya waziri mkuu huyo wa New Zealand ni miongoni mwa shutuma kali alizotoa dhidi ya Netanyahu na huenda zikawa ni jibu kwa vyama vya upinzani vinavyosema kuwa serikali ya nchi hiyo imebakia nyuma katika kulitambua taifa la Palestina.
New Zealand imetangaza kuwa, itaamua mwezi Septemba iwapo itaitambua Palestina kama taifa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Wazayuni wanaofanya safari nchini New Zealand wapo chini ya uangalizi na darubini kali na kufanya mazingira kuwa magumu kwa wale ambao wana historia kuhudumu katika jeshi la Kizayuni.
Idara ya uhamiaji ya serikali ya New Zealand imewataka Waisraeli wanaoomba visa kutoa maelezo kama wamewahi kuhudumu katika kijeshi kama sharti la kuingia nchini humo, liliripoti gazeti la Times of Israel.
Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji ya New Zealand, Mzayuni yeyote ambaye ana historia ya kuhudumu katika jeshi la Iisrael hatopatiwa visa ya kuingia katika nchi hiyo.
Katika siku za hivi karibuni kumewasilishwa mashtaka dhidi ya wanajeshi wa Israel katika nchi mbalimbali zikiwemo Brazil, Argentina na Sri Lanka jambo ambalo limezidisha wasi wasi wa utawala wa Kizayuni kuhusu kufuatiliwa kisheria wanajeshi wa Israel kote duniani.