Mazungumzo ya mkataba wa plastiki yakabiliwa na mkwamo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129568
Mazungumzo ya mjini Geneva Uswisi ya kutafuta mkataba wa kwanza duniani kisheria ambao utashughulikia uchafuzi wa plastiki, yamelazimika kusogezwa mbele baada ya kufikia muda wa mwisho bila maelewano.
(last modified 2025-08-15T11:11:48+00:00 )
Aug 15, 2025 11:10 UTC
  • Nchi 34 kati ya 54 barani Afrika zimepitisha sheria ya kupiga marufuku plastiki na kuitekeleza au kupitisha sheria kwa nia ya utekelezaji.
    Nchi 34 kati ya 54 barani Afrika zimepitisha sheria ya kupiga marufuku plastiki na kuitekeleza au kupitisha sheria kwa nia ya utekelezaji.

Mazungumzo ya mjini Geneva Uswisi ya kutafuta mkataba wa kwanza duniani kisheria ambao utashughulikia uchafuzi wa plastiki, yamelazimika kusogezwa mbele baada ya kufikia muda wa mwisho bila maelewano.

Siku kumi za mazungumzo mjini Geneva zilipaswa kukamilika jana lakini zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya muda wa mwisho, mwenyekiti wa mazungumzo ya Kamati ya Kimataifa ya Majadiliano (INC) ya Umoja wa Mataifa, Luis Vayas Valdivieso, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba mazungumzo hayo yamesogezwa mbele hadi leo Ijumaa.

Baada ya siku kadhaa za majadiliano makali, kumekuwa na matumaini kwamba kambi pinzani, huenda zikatatua tofauti zake na kufikia makubaliano ya mkataba wa kimataifa wa kukabiliana na janga la plastiki ambalo linachafua ardhi, bahari na mazingira ya watu.

Hadi kufikia Alhamisi usiku, nchi zilikuwa zikingoja rasimu mpya ambayo ingeweza kuwa msingi wa mazungumzo zaidi baada ya wajumbe wanaotaka mkataba kabambe wa plastiki kuutupilia mbali ule uliopendekezwa Jumatano.

Mwanaharakati wa kupinga matumizi ya plastiki jijini Nairobi, Kenya

 

Mataifa yanayoshinikiza upatikanaji wa mkatabawa kina, ikiwemo Panama, Kenya, Uingereza na Umoja wa Ulaya, yalionyesha kushangazwa kwamba maandishi muhimu juu ya mzunguko wa uchafuzi wa plastiki, kuanzia uzalishaji hadi utupaji wa taka pamoja na madhara kwa afya, yalikuwa yameondolewa kabisa kutoka kwenye rasimu. Mzungumzaji mkuu wa Panama Juan Carlos Monterrey ameelezea kutoridhishwa na rasimu hiyo.

Bado kuna tofauti kadha baina ya nchi, ikiwa ni pamoja na mataifa yanayozalisha mafuta kupinga kuwekewa ukomo wa utengenezaji plastiki zitokanazo na mafuta ya petroli, makaa ya mawe na gesi, huku makundi kadhaa ikiwemo Umoja wa Ulaya na nchi za visiwa yakishinikiza ukomo wa uzalishaji plastiki, pamoja na udhibiti mkali wa bidhaa za plastiki na kemikali hatari.