Idadi ya waliofariki dunia kwa mafuriko Pakistan yapindukia 300
Idadi ya watu waliopoteza maisha yao kufuatia janga la mafuriko nchini Pakistan imeongezeka na kufikia 337.
Waokoaji kaskazini-magharibi mwa Pakistan wameopoa miili mingine 63 kutoka kwa nyumba zilizobomolewa na mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kuongeza idadi ya vifo kutokana na maporomoko hayo kufikia takriban 337.
Msemaji wa huduma za dharura Mohammad Suhail amesema kuwa, mamia ya maafisa wa uokoaji bado wanatafuta manusura katika eneo la Buner, mojawapo ya wilaya zilizoathirika katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, ambapo mvua kubwa ilisababisha mafuriko makubwa jana Ijumaa.
Kulingana na naibu kamishna wa Buner Kashif Qayyum, maafisa hao wa uokoaji pia wamekuwa wakijaribu kutafuta miili katika vijiji vilivyoathirika vibaya zaidi vya Pir Baba na Malik Pura, ambapo watu wengi walikufa hiyo jana.
Katika tukio jingine, helikopta iliyokuwa imebeba vifaa vya misaada imeanguka na kusababisha vifo vya wahudumu watano wakiwemo marubani wawili mkoani Khyber Pakhtunkhwa kaskazini magharibi mwa Pakistani.
Mamlaka ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa imesema watu wengine wengi bado hawajulikani walipo.
Vifo vimeripotiwa pia katika mkoa wa Gilgit-Baltistan na Kashmir inayosimamiwa na Pakistan inayojulikana kama Azad Jammu na Kashmir.
Timu za uokoaji zimesema, mvua hizo zilisababisha mafuriko makubwa katika eneo la Salarzai wilayani Bajaur siku ya Ijumaa asubuhi na kusomba nyumba kadhaa.
Mamlaka za maeneo hayo zimewahamishia watu wengi kwenye maeneo salama kutokana na mvua na maporomoko ya ardhi huko Khyber Pakhtunkhwa na eneo la Gilgit-Baltistan.
Mvua za monsuni, ambazo kwa kawaida hunyesha kuanzia Juni hadi Septemba, mara nyingi husababisha hasara na uharibifu kote Asia Kusini, ikiwa ni pamoja na Pakistan, lakini katika miaka ya karibuni mabadiliko ya tabianchi yameongeza hali ya kutotabirika unyeshaji wake na nguvu yake.