‘Haikubaliki’: Australia yaikosoa Israel kwa kubatilisha visa za maafisa wake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129732-haikubaliki’_australia_yaikosoa_israel_kwa_kubatilisha_visa_za_maafisa_wake
Australia imeikosoa Israel kwa kubatilisha visa za mabalozi wake waliokuwa na mamlaka kwa Mamlaka ya Wapalestina, hatua iliyotambuliwa kama ulipizaji kisasi baada ya Canberra kukataa kumkaribisha mwanasiasa wa mrengo wa kulia wa Israel.
(last modified 2025-08-19T23:07:18+00:00 )
Aug 19, 2025 23:07 UTC
  • ‘Haikubaliki’: Australia yaikosoa Israel kwa kubatilisha visa za maafisa wake

Australia imeikosoa Israel kwa kubatilisha visa za mabalozi wake waliokuwa na mamlaka kwa Mamlaka ya Wapalestina, hatua iliyotambuliwa kama ulipizaji kisasi baada ya Canberra kukataa kumkaribisha mwanasiasa wa mrengo wa kulia wa Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Penny Wong, amekosoa hatua ya kubatilishwa visa siku ya Jumanne, akiitaja kuwa “jibu lisilo na msingi” ambalo limeongeza kutengwa utawala wa Israel.

Ameongeza kuwa, hatua kama hizi kutoka kwa baraza la mawaziri la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, pia zinadhoofisha diplomasia na juhudi za kimataifa kuelekea kwenye amani.

Australia ilikuwa imempiga marufuku Simcha Rothman, mwanasiasa mwenye misimamo mikali aliye karibu na muungano wa Netanyahu, ambaye ameunga mkono waziwazi mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Rothman alikuwa amepangwa kutoa hotuba kadhaa nchini Australia.

Ndani ya masaa machache, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, alitangaza kubatilishwa visa za maafisa wa ubalozi wa Australia.

Aidha ameuagiza ubalozi wa Israel huko Canberra kufanya ukaguzi mkali zaidi kwa maombi yoyote ya visa ya maafisa wa Australia siku za usoni.

Saar amesema hatua hiyo pia ni majibu kwa uamuzi wa awali wa serikali ya Australia kutangaza nia ya kutambua nchi ya Palestina kwenye mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba.

Nchi nyingi, zikiwemo washirika wa Israel kama Ufaransa, zimetangaza mipango kama hiyo ya kutambua rasmi Palestina kama nchi huru.

Hatua ya kutambuliwa Palestina ni pigo kwa utawala dhalimu wa Israel ambao  kwa miongo kadhaa umekuwa ukitekeleza mashambulizi dhidi ya Wapalestina na kunyakua ardhi zao, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya 62,000 Wapalestina, wengi wakiwa wanawake na watoto.

Gaza

Wakiunga mkono uwezekano wa kutambuliwa rasmi Palestina kama nchi huru, wachambuzi wamesisitiza umuhimu wa washirika wakuu wa Israel kusitisha mara moja kutoa silaha zisizo na kikomo kwa Tel Aviv, ambazo zimeonekana kuwa sababu kuu ya mpango wake wa kuendeleza mauaji ya kimbari huko Palestina.