Waziri Mkuu wa India 'apuuza' simu 4 za Trump huku vita vya kibiashara vya Marekani vikiendelea
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ameripotiwa kupuuza majaribio kadhaa ya Donald Trump ya kumtafuta kwa simu huku vita vya kibiashara kati ya nchi hizo vikipamba moto, ambavyo vimechochewa na ushuru mzito wa forodha wa rais wa Marekani dhidi ya bidhaa kutoka India.
Kwa mujibu wa jarida la Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani, Trump amejaribu mara nne katika wiki za hivi karibuni kumpata Modi kwenye laini ya simu, lakini waziri mkuu wa India amekataa kujibu.
Ripoti hiyo imetolewa wakati Ikulu ya White House ikianzisha awamu mpya ya adhabu, ambayo ni ushuru mpya wa asilimia 25 kwa bidhaa za India, juu ya hatua za hapo awali, na kupandisha juu kiwango cha ushuru huo kwa ujumla hadi asilimia 50.
Washington imesema hatua hiyo, ni jibu la moja kwa moja kwa ununuzi wa India wa mafuta ya Russia.
Mnamo Agosti 24, gazeti la Nikkei Asia la Japani pia lilitoa ripoti kama hiyo, likiwanukuu wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wa India ambao walisema, hivi karibuni Trump alifanya "majaribio kadhaa" ya kumpigia simu Modi bila mafanikio.
Waliongeza kuwa Modi amekataa kupokea simu ya Trump mara kadhaa, na kuzidisha hasira ya Trump.
Trump anasema kwamba uhusiano mkubwa wa kibiashara baina ya New Delhi na Moscow ni sawa na "kuchochea vita," akijaribu kudai kwamba mchango wa India katika uchumi wa Russia unazidisha mzozo nchini Ukraine.