Mjumbe wa Trump akosolewa vikali kwa kuwataka waandishi habari waache "uhayawani"
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130060-mjumbe_wa_trump_akosolewa_vikali_kwa_kuwataka_waandishi_habari_waache_uhayawani
Kejeli za matusi ya ubaguzi wa rangi kutoka kwa mjumbe wa kikanda wa Marekani dhidi ya waandishi wa habari wa Lebanon zimezusha wimbi la ukosoaji miongoni mwa watu wengi wanaotembelea mitandao ya kijamii, wakiwemo wanaharakati wanaopinga ukoloni na watu mashuhuri wa Lebanon.
(last modified 2025-08-27T10:41:48+00:00 )
Aug 27, 2025 10:41 UTC
  • Tom Barrack
    Tom Barrack

Kejeli za matusi ya ubaguzi wa rangi kutoka kwa mjumbe wa kikanda wa Marekani dhidi ya waandishi wa habari wa Lebanon zimezusha wimbi la ukosoaji miongoni mwa watu wengi wanaotembelea mitandao ya kijamii, wakiwemo wanaharakati wanaopinga ukoloni na watu mashuhuri wa Lebanon.

Mjumbe wa Rais Donald Trump kuhusu Syria na balozi wa Washington nchini Uturuki, Tom Barrack alizua ghadhabu kubwa baina ya watu, jana Jumanne, baada ya kuwaambia waandishi wa habari waliojaribu kumuuliza maswali wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Beirut "wanyamaze" na kuacha "uhayawani."

"Kuweni na mienendo ya watu waliostaarabika" alisema Tom Barrack kuwaambia waandishi wa habari waliokuwa wakimuuliza maswali.

Afisa huyo aliendelea kudai kuwa hali katika eneo la Asia Magharibi - ambako uchokozi wa Israel na Marekani umegharimu maisha ya maelfu ya watu na kusababisha machafuko makubwa - imetokana na mienendo ambayo amewashutumu waandishi wa habari kuwa ndio tabia na mazoea yao.

Wanaharakati wa majukwaa ya mitandao ya kijamii, wamelaani matamshi ya "kikoloni" ya Barrack, waliyoyataja kuwa yamejaa jeuri na ni ya kibaguzi kupita kiasi.

Mwanaharakati aliyejitambulisha kama Thomas Keith amesema matamshi ya mjumbe huyo wa Rais Donald Trump "yanaakisi tabia halisi ya kikoloni." 

Keith ameongeza kuwa, afisa huyo wa Marekani hakuwa katika nafasi ya kuweka "sheria" za jinsi wenyeji wanapaswa kuzungumza katika nchi yao wenyewe."

Mchambuzi wa masuala ya kijiografia, Kevork Almassian pia amesema matamshi ya Barrack yanatokana na tabia ya kujiona juu na bora ya wakoloni.

"Tom Barrack ameenda mbali hadi kuwaonya waandishi wa habari wa Lebanon kutokuwa "wanyama" na kuwataka "kuwa wastaarabu" - akidai hili ndilo tatizo la kanda ya Magharibi mwa Asia", amesema Kevork Almassian na kuongeza kuwa: Hii sio diplomasia. Ni kujikuza kwa kikoloni..

Mwandishi wa habari wa Mlebanon-Mwingereza na mwandishi wa zamani wa Sunday Times, Hala Jaber amemfananisha Tom Barrack na "kamishna wa kikoloni wa karne ya 19." "Hauendeshi nchi hii, na huwezi kuwatukana watu wake," aliongeza.

Wakati huo huo, mwandishi na mshairi wa Kipalestina, Mosab Abu Toha, amesema ni utawala wa Israel na muungaji mkono wake mkuu kijeshi na kisiasa, Marekani, ambao ndio wenye mienendo na tabia za "kinyama na kihayawani."