Guterres: Hali mbaya ya Ghaza hailingani na hali yoyote katika zama za hivi karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130148-guterres_hali_mbaya_ya_ghaza_hailingani_na_hali_yoyote_katika_zama_za_hivi_karibuni
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa indhari kali ya kuongezeka vifo vya raia huko Ghaza, akiielezea hali ya eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro na Israel kuwa "haijafanana na yoyote katika zama za hivi karibuni."
(last modified 2025-10-19T03:07:26+00:00 )
Aug 29, 2025 07:36 UTC
  • Guterres: Hali mbaya ya Ghaza hailingani na hali yoyote katika zama za hivi karibuni

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa indhari kali ya kuongezeka vifo vya raia huko Ghaza, akiielezea hali ya eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro na Israel kuwa "haijafanana na yoyote katika zama za hivi karibuni."

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini New York siku ya Alkhamisi, Guterres amezungumzia uharibifu wa kimpangilio unaofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel huko Ghaza wa dhidi ya mifumo ya chakula, maji na huduma za afya, ambayo imewaacha watu wakikabiliwa na baa la njaa.

Katibu Mkuu wa UN ameelezea pia wasiwasi alionao juu ya uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Israel katika Jiji la Ghaza, na kubainisha kuwa unaakisi ongezeko kubwa la vitendo vya uhasama.

"Mamia ya maelfu ya raia - ambao tayari wamechoka na wamepatwa na kiwewe - watalazimika kukimbia kwa mara nyingine, na kuziingiza familia katika hatari kubwa zaidi. Hili ni lazima likome," amesisitiza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Kadhalika amesema: "Ghaza imerundikwa na vifusi, miili, na uwezekano wa ukiukaji zaidi wa sheria za kimataifa," na akaonya kwamba baa la njaa sasa ndiyo hali halisi ya wakati huu ni si tishio la siku za usoni.

Guterres ameeleza bayana kuwa hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa Ghaza ni matokeo ya vitendo vya makusudi vinavyopuuza haki za msingi za binadamu.

Ameutaka utawala wa kizayuni wa Israel, ukiwa ni mamlaka inayokalia ardhi kwa mabavu, utimize wajibu wake kwa kudhamini utoaji wa vifaa muhimu kama vile chakula, maji na dawa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amehitimisha kwa ujumbe mzito akisema: "kuwatesa kwa njaa raia kusitumike katu kuwa mbinu ya kupigana vita. Raia lazima walindwe, na ufikishaji misaada ya kibinadamu lazima ufanywe bila kuzuiliwa. Hakuna visingizio zaidi vya kutoa. Hakuna vizuizi zaidi vya kuwekwa. Hakuna uwongo tena wa kusema"…/