UN yasema Marekani inapaswa kuondoa vikwazo dhidi ya wanadiplomasia wa Iran
-
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq
Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa Marekani inalazimika kuwawezesha wanadiplomasia wa Iran walioidhinishwa kutekeleza majukumu yao bila vizuizi, ukikumbusha msimamo wa taasisi hiyo kwamba Washington, kama nchi mwenyeji, ina wajibu wa kuruhusu harakati zisizo na mipaka kwa maafisa wote wa kidiplomasia walioko katika makao makuu ya UN.
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, alitoa kauli hiyo Alhamisi wakati wa mkutano na waandishi wa habari, alipoulizwa iwapo Umoja wa Mataifa umepokea taarifa rasmi kutoka Jamhuri ya Kiislamu kuhusu kuongezwa kwa masharti dhidi ya Ujumbe wake wa Kudumu.
Alisema: “Kila mara mataifa yanapokumbana na vikwazo dhidi ya wanadiplomasia wao, hulifikisha suala hilo kwetu, nasi tunakumbusha nchi mwenyeji wajibu wake chini ya Mkataba wa Nchi Mwenyeji kuruhusu uhuru wa kutembea kwa wanadiplomasia walioidhinishwa katika Umoja wa Mataifa.”
Haq alisisitiza msimamo wa kudumu wa taasisi hiyo, akibainisha: “Mtazamo wetu kuhusu mataifa yote, si Iran pekee, ni kuhakikisha nchi mwenyeji inawawezesha wanadiplomasia wake kufanya kazi zao bila kubanwa, pindi tu wanapoidhinishwa hapa.”
Tehran imeikosoa vikali Marekani kwa kuongeza shinikizo dhidi ya Ujumbe wake katika UN.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilishutumu Washington kwa kutumia vibaya hadhi yake ya “nchi mwenyeji” kwa kuweka vikwazo vingi dhidi ya makazi, harakati, huduma za kibenki, na hata manunuzi ya kila siku ya wanadiplomasia wa Iran.
Ilisema hatua hizo zimepangwa mahsusi kuvuruga majukumu ya kawaida na ya kisheria ya wawakilishi wa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa Washington kuzuia wanadiplomasia watatu wa Ujumbe wa Iran kuendelea na kazi zao ni “kilele” cha ukiukaji wa Marekani dhidi ya Mkataba wa Nchi Mwenyeji.
Wizara hiyo imelaani hatua hiyo kama isiyo halali, yenye malengo ya kisiasa, na ukiukaji unaoibua maswali kuhusu uhalali wa Marekani kuendelea kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Ilionya kuwa hatua kama hizo zinadhoofisha ufanisi wa UN, zinatia doa itibari Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, na zinakwenda kinyume na misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Mzozo huu mpya unafuatia malalamiko ya Iran mwezi Septemba, wakati Balozi wake katika UN, Amir Saeid Iravani, alipolalamikia vikwazo vya Marekani dhidi ya safari ya Rais Masoud Pezeshkian, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi, na maafisa wengine waandamizi waliokuwa wakihudhuria Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.