Ukosoaji waongezeka kuhusu afya ya Trump baada ya kuonekana mchovu hadharani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134260-ukosoaji_waongezeka_kuhusu_afya_ya_trump_baada_ya_kuonekana_mchovu_hadharani
Mjadala kuhusu afya ya Rais wa Marekani Donald Trump umechacha upya baada ya matukio kadhaa ya hadharani ambapo alionekana mchovu au kusinzia, hali iliyozua maswali mapya kuhusu uwezo wake kiafya katika umri wake wa miaka 79.
(last modified 2025-12-13T11:18:16+00:00 )
Dec 13, 2025 11:18 UTC
  • Rais Trump alionekana kama vile amesinzia wakati wa hafla katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House, tarehe 6 Novemba 2025
    Rais Trump alionekana kama vile amesinzia wakati wa hafla katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House, tarehe 6 Novemba 2025

Mjadala kuhusu afya ya Rais wa Marekani Donald Trump umechacha upya baada ya matukio kadhaa ya hadharani ambapo alionekana mchovu au kusinzia, hali iliyozua maswali mapya kuhusu uwezo wake kiafya katika umri wake wa miaka 79.

Katika tukio moja Ikulu ya White House, kamera zilimnasa akifumba macho kwa sekunde kadhaa wakati Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio akitoa taarifa ya sera za nje. Ingawa haijathibitishwa kama alilala kwa muda mfupi, tukio hilo limeongezea wasiwasi uliokuwepo tayari.

Ikulu imeendelea kupuuzilia mbali hoja hizi, ikisisitiza kuwa rais yuko salama kiafya, lakini tetesi zimeongezeka kutokana na michubuko inayoonekana mikononi mwake, taarifa za kusinzia katika vikao, na ratiba yake ya kazi kupungua ikilinganishwa na muhula wake wa kwanza.

Katika kumbukumbu ya Septemba 11 Pentagon, video iliyomuonyesha upande wa kulia wa uso wake ukidondoka kidogo ilizua uvumi wa mtandaoni kuhusu uwezekano wa kupata kiharusi, madai ambayo utawala wake ulipinga vikali.

Ripoti ya New York Times iliyohoji masuala haya ilimfanya Trump kujibu kwa ukali, akiituhumu kwa uchochezi na hata usaliti kupitia ujumbe mrefu kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Truth Social. Trump, rais mzee zaidi kuwahi kuapishwa Marekani, amejigamba kuwa vipimo vyake vya afya ni imara na hakuna rais aliyewahi kufanya kazi kwa bidii kama yeye.

Ikulu imeeleza kuwa michubuko mikononi mwake inatokana na kusalimiana mara kwa mara na wananchi, ingawa baadhi ya madaktari wamehoji maelezo hayo, wakisema yanaweza kutokana na sababu mbalimbali za kitabibu.

Daktari Boback Berookhim wa New York amesisitiza kuwa maafisa wanaficha jambo kuhusiana na afya ya Trump. Rekodi za White House zinaonyesha kuwa ratiba ya Trump sasa huanza kuchelewa zaidi kuliko ilivyokuwa muhula wake wa kwanza, na idadi ya matukio rasmi aliyohudhuria mwaka huu ni ndogo zaidi kuliko mwaka 2017.