Idadi ya watu waliokufa katika mafuriko Indonesia yapindukia 1000
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134282-idadi_ya_watu_waliokufa_katika_mafuriko_indonesia_yapindukia_1000
Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na janga la mafuriko nchini Indonesia imeongezeka na kupindukia 1000.
(last modified 2025-12-14T07:09:46+00:00 )
Dec 14, 2025 07:09 UTC
  • Idadi ya watu waliokufa katika mafuriko Indonesia yapindukia 1000
    Idadi ya watu waliokufa katika mafuriko Indonesia yapindukia 1000

Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na janga la mafuriko nchini Indonesia imeongezeka na kupindukia 1000.

Ripoti kutoka nchini humo zinasema, mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 nchini Indonesia. Hayo yameelezwa na maafisa wa uokoaji nchini humo.

Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Maafa limesema katika taarifa yake kwamba, maafa hayo, ambayo yamekumba kisiwa cha kaskazini-magharibi cha Sumatra katika muda wa wiki mbili zilizopita, yamesababisha vifo vya watu 1003, huku 218 hawajulikani walipo na wengine zaidi ya 5,400 wamejeruhiwa.

Baada ya kuzuru eneo la Langkat katika mkoa wa Kaskazini wa Sumatra hii leo, Rais wa nchi hiyo Prabowo Subianto amesema hali imeimarika na maeneo kadhaa ambayo yalikuwa yamekatwa na mafuriko na maporomoko hayo sasa yanafikika.

Gharama za ujenzi mpya baada ya maafa hayo zinaweza kufikia dola bilioni 3.1 na hadi kufikia sasa, serikali ya Indonesia imepuuza mapendekezo ya kuomba msaada wa kimataifa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mafuriko mabaya yaliyozikumba nchi za Indonesia, Sri Lanka, Thailand na Malaysia mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba, yalipelekea zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha katika kipindi cha chini ya wiki moja. Kwa uchache watu 502 waliripotiwa kufariki dunia nchini Indonesia, 335 nchini Sri Lanka, 176 nchini Thailand na watatu nchini Malaysia.