Israel: Tutampa Trump ushahidi wa kuhusika Obama na azimio la UNSC
Utawala wa Kizayuni wa Israel umedai kuwa una ushahidi madhubuti unaothibitisha kuwa Rais wa Marekani Barack Obama alihusika kikamilifu na kupitishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni; na kwamba nyaraka na ushahidi huo utampatia rais mteule wa Marekani tu Donald Trump.
Balozi wa utawala haramu wa Israel nchini Marekani Ron Dermer ameiambia kanali ya televisheni ya CNN kuwa watamtaarifu rais ajaye wa Marekani suala hilo wakati atakapoingia madarakani na yeye ataamua kama kutakuwa na haja ya wananchi wa Marekani kulielewa suala hilo.
Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu alimshutumu Obama kwa "kula njama" na Wapalestina na kumwita balozi wa Marekani aliyeko Tel Aviv.
Hata hivyo serikali ya Marekani inayomaliza muda wake imekanusha madai kwamba imehusika na hatua iliyochukuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupitisha azimio linaloilaani Israel na kuitaka isitishe mara moja na kikamilifu ujenzi wa vitongoji.
Utawala haramu wa Israel umekuwa ukikaidi kila mara kutekeleza wito wa jamii ya kimataifa yakiwemo maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kuutaka usimamishe ujenzi na upanuzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu; suala ambalo linatajwa kama moja ya sababu kuu za kuvunjika kile kinachoitwa mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati mwaka 2014…/