Katibu Mkuu wa UN: Tuna dunia moja pekee, tunapaswa kuilinda
https://parstoday.ir/sw/news/world-i84402-katibu_mkuu_wa_un_tuna_dunia_moja_pekee_tunapaswa_kuilinda
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema, sayari dunia ndio makazi pekee ya watu, akimaanisha kuwa hakutakuwa na pa kukimbilia ikiwa itachafuliwa na kusisitiza kwamba “ni muhimu kulinda afya ya anga yake, utajiri, na aina mbalimbali ya viumbe vilivyoko duniani bila kusahau ikolojia yake na rasilimali lukuki.”
(last modified 2026-04-23T06:05:17+00:00 )
Jun 05, 2022 03:46 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Tuna dunia moja pekee, tunapaswa kuilinda

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema, sayari dunia ndio makazi pekee ya watu, akimaanisha kuwa hakutakuwa na pa kukimbilia ikiwa itachafuliwa na kusisitiza kwamba “ni muhimu kulinda afya ya anga yake, utajiri, na aina mbalimbali ya viumbe vilivyoko duniani bila kusahau ikolojia yake na rasilimali lukuki.”

Katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Mazingira Duniani, Guterres amesisitiza kwa kusema, "tunaibebesha dunia mzigo mkubwa wa kujilinda kwa njia ambayo si endelevu. Mifumo asili ya dunia haiwezi kuenda na kasi ya matakwa yetu.”

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kinachoharibika si dunia pekee, bali binadamu pia wanadhurika na kwamba mazingira yenye afya ni muhimu kwa ajili ya watu wote na kwa ajili ya malengo 17 ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katibu Mkuu wa UN amesema mazingira yenye afya, “hutupatia chakula, maji safi, dawa, na hurekebisha hali za kupitiliza za tabia nchi, halikadhalika huepusha majanga makali ya hali ya hewa,”

Ni kwa mantiki hiyo Guterres amesema ni muhimu sana kusimamia kwa ukamilifu mazingira na kuhakikisha huduma zake zinafikia pia watu wote hususan jamii zilizo hatarini zaidi.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni 3 wameathiriwa na kumomonyoka kwa mifumo ya ikolojia.

Uchafuzi wa hewa unasababisha watu milioni 9 kufariki dunia kabla ya kutimiza umri wa miaka 75, na kwa mimea na baadhi ya aina za wanyama viko hatarini kutoweka ndani ya miongo michache.

Aidha imeelezwa kuwa, takribani nusu ya wakazi wa dunia wako katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi—sawa na mara 15 zaidi ya kufa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kama vile joto kupindukia, mafuriko na ukame.../