UN: Teknolojia ya intaneti inatumiwa vibaya katika Usafrishaji Haramu wa Binadamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, migogoro, janga la tabianchi, ukosefu wa usawa na umasikini huwaacha mamilioni ya watu katika hatari ya wahalifu wanaotumia vibaya mtandao kuwahadaa waathiriwa wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu kwa ahadi za uwongo.
Antonio Guterres ameyasema hayo katika ujumbe aliotoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu inayoadhimishwa Julai 30 kila mwaka.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “matumizi na matumizi mabaya ya teknolojia” katika kutekeleza uhalifu huo unaoathiri maelfu ya wanawake, watoto na wanaume kila mwaka.
Imeelezwa kuwa, takribani kila nchi duniani imeathiriwa na biashara haramu ya binadamu kama sehemu ya kufikia, asili au njia ya kupita.
Wahanga wengi wanadanganywa na walanguzi wa binadamu hasa kwenye mtandao.
Guterres amekumbusha katika ujumbe wake kuhusu janga la Covid-19 ambalo liliwatenganisha watoto na vijana kutoka kwa marafiki na wenzao na akaongezea kwa kusema: “kwa hiyo, walitumia muda mwingi wakiwa peke yao mtandaoni.”
Katibu Mkuu wa UN amesema, wahalifu wanachukua fursa ya dosari na udhaifu huo kufuatilia, kudhibiti na kuwanasa waathiriwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu ili kuwabaini.
Katika ujumbe wake, Guterres ametanabahisha pia kuwa tatizo hilo linazidi kuwa baya zaidi, hasa kwa wasichana na wanawake, ambao ndio wahanga wengi wa magendo ya binadamu duniani kote.
Takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC zinaonyesha kuwa, katika mwaka 2018 watu 50,000 waligunduliwa kuwa waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu katika nchi 148 duniani.
Nusu ya waathiriwa hao walisafirishwa kwa madhumuni ya ngono na asilimia 38 walinyonywa katika kazi za kulazimishwa.
Ulimwenguni kote, mmoja kati ya watu watatu walioathiriwa ni mtoto. Idadi ya watoto imeongezeka mara tatu, na idadi ya wavulana imeongezeka kwa asilimia 500 katika miaka mitano iliyopita.
Siku ya Kimataifa ya Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu ilitangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika azimio la mwaka 2013.../