UN yailaumu Ukraine kwa kuwanyanyasa mateka wa vita wa Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93918-un_yailaumu_ukraine_kwa_kuwanyanyasa_mateka_wa_vita_wa_russia
Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Ukraine dhidi ya mateka wa kivita wa Russia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2023 03:54 UTC
  • UN yailaumu Ukraine kwa kuwanyanyasa mateka wa vita wa Russia

Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Ukraine dhidi ya mateka wa kivita wa Russia.

Marta Hurtado, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, amesema kwamba shirika hilo limeelezea wasiwasi wake juu ya unyanyasaji wa wafungwa wa kivita wa Russia huko Ukraine katika mazungumzo yake na Oleksii Reznikov , Waziri wa Ulinzi wa Ukraine. 

Mapema wiki hii, ilisambazwa video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wanajeshi wa Ukraine wakiwanyonga na kuwaua wafungwa wa kivita wa Russia.

Mwezi Novemba mwaka jana pia Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza kuwa wanajeshi wa Ukraine wanafanya mauaji ya kikatili dhidi ya mateka wa kivita wa Russia.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imelaani mauaji hayo ya mateka wa vita yanayofanywa na wanajeshi wa Ukraine na imezitaka jumuiya za kimataifa kulaani vikali ukatili huo na kufanya uchunguzi kamili kuhusiana na jinai hiyo.

Wakati huo Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza habari ya kunyongwa mateka 10 wa kivita wa Russia huko Ukraine na kuishutumu Kiev kuwa imefanya uhalifu wa kivita, ambao kwa mujibu wa Moscow, umefumbiwa macho na nchi za Magharibi.

Wizara ya Ulinzi ya Russia inasema, mauaji ya kikatili dhidi ya wanajeshi wa Russia waliotekwa Ukraine sio kesi ya kwanza ya aina hiyo na kwamba hilo limekuwa jambo la kawaida linalofanywa na wajeshi wa Ukraine waungwa mkono kikamilifu na utawala wa Kiev na kufumbiwa macho na waitifaki wake wa Magharibi.