May 14, 2023 11:27 UTC
  • Chama cha Modi chang'olewa Karnataka, jimbo la India lililopiga marufuku Hijabu

Chama cha upinzani cha Congress nchini India kimeshinda katika uchaguzi wa jimbo muhimu la Karnataka kusini mwa nchi hiyo na kuking'oa chama tawala cha Waziri Mkuu Narendra Modi, BJP mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa kitaifa.

Chama cha Congress kimehitimisha uongozi wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) cha Modi katika jimbo hilo la Karnataka, ambalo ni jimbo pekee la kusini lililokuwa likidhibitiwa na kikundi cha kitaifa cha Kihindu.

Wakati matokeo rasmi yanakaribia kutangazwa, chama cha Congress tayari kimeshashinda nafasi 114 katika bunge la viti 224, vya kutosha kwa wingi wa jumla.

Jimbo la Karnataka lina idadi ya zaidi ya watu milioni 60 - sawa na Uingereza - na mji mkuu wake Bengaluru ni kitovu cha teknolojia cha India.

Karnataka linakuwa jimbo la pili kwa chama cha Modi kupoteza kwa chama cha Congress katika miezi sita iliyopita. Mnamo Desemba 2022, Congress iliiondoa BJP kaskazini mwa Himachal Pradesh, jimbo dogo lililoko kwenye eneo la Himalaya.

Kiongozi wa chama cha Congress, Rahul Gandhi

Matokeo ya kura za uchaguzi wa jimbo la Karnataka yanatarajiwa kuupa nguvu upinzani uliogawanyika kwa kiasi kikubwa ambao unapania kuunda umoja wa kupambana na Modi katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ambapo kiongozi huyo mwenye misimamo mikali ya Kihindu na ya chuki dhidi ya Waislamu atawania kuchaguliwa tena kuwa waziri mkuu wa India kwa muhula wa tatu mfululizo.

Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, chama cha Modi kimejaribu kujizatiti zaidi katika jimbo la Karnataka, ambako mgawanyiko wa kijamii kati ya Wahindu walio wengi na Waislamu walio wachache umeongezeka baada ya viongozi na wafuasi wa BJP kuwapiga marufuku wasichana Waislamu kuvaa hijabu kama sehemu ya sare zao za skuli.

Kiongozi wa chama cha Congress Rahul Gandhi amewaambia wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakisherehekea ushindi wa chama chao mjini New Delhi kwamba, kwa ushindi kiliopata chama hicho huko Karnataka "Masoko ya chuki yameshafungwa na maduka ya upendo yamefunguliwa".../

Tags