Guterres ataka kuundwa taasisi ya kudhibiti Akili Mashine (AI)
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98720-guterres_ataka_kuundwa_taasisi_ya_kudhibiti_akili_mashine_(ai)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za makusudi za kuzuia kuenea kwa matumizi mabaya ya zana za teknolojia ya akili mashine (AI), huenda teknolojia hiyo ikageuka na kuwa zimwi lisilodhibitika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2023 03:23 UTC
  • Guterres ataka kuundwa taasisi ya kudhibiti Akili Mashine (AI)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za makusudi za kuzuia kuenea kwa matumizi mabaya ya zana za teknolojia ya akili mashine (AI), huenda teknolojia hiyo ikageuka na kuwa zimwi lisilodhibitika.

Antonio Guterres alitoa indhari hiyo jana Jumatatu na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa dunia kuunda mifumo na sheria za kuzuia matumizi mabaya ya teknolojia hiyo ya Artificial Intelligence.

Guterres ameeleza bayana kuwa, kuna udharura wa kubuniwa kanuni na miongozo kwa serikali, kampuni za teknolojia, na mashirika ya matangazo ya biashara ili yaweze kudhibiti uenezaji wa taarifa za urongo, za chuki na matumizi mabaya ya teknolojia ya akili bandia.

Amesema anapanga kuunda Bodi ya Ushauri ya Kisayansi ndani ya siku chache zijazo, na Bodi ya Ushauri ya Akili Mashine kufikia Septemba mwaka huu, ili ziandae ramani ya njia na muelekeo utakaochukuliwa na UN juu ya kadhia hiyo.

Onyo la Katibu Mkuu wa UN limekuja wiki chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutahadharisha pia kuhusu hatari ya matumizi mabaya ya akili mashine (AI).

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN

Kwa mujibu wa WHO, roboti zinazoundwa na akili bandia zinaweza kutumiwa vibaya kuzalisha na kusambaza taarifa za uongo zenye kushawishi kwa njia ya maandishi, sauti au maudhui ya video ambayo ni vigumu kwa umma kutofautisha na maudhui salama na ya kuaminika.

Tangu kutolewa kwa roboti ya akili bandia ya "ChatGPT" Novemba mwaka jana, mjadala kuhusu hatari zinazosababishwa na akili bandia (AI) umeongezeka katika tasnia ya viwanda na duru za wasomi.