Ijumaa, Julai 21, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 3 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria sawa na 21 Julai mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW aliwatumia barua wafalme wa tawala mbalimbali duniani, na kwa hatua hiyo akawa ameanza rasmi kuwalingania watu Uislamu kimataifa.
Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume wa Mwenyezi Mungu alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa duniani bila wasiwasi.
Wanahistoria wanasema kuwa, Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine makubwa katika zama hizo ambapo kila mmoja kati ya watawala hao alitoa jibu lake. Hatua hiyo ya Mtume ilionesha wazi kuwa dini ya Uislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.
Miaka 1384 iliyopita yaani tarehe 3 Muharram mwaka 61 Hijria, jeshi la Umar bin Saad liliwasili katika ardhi ya Karbala.
Baada ya Hurr bin Yazid kumzingira Imam Hussein AS na maswahaba wake katika ardhi ya Karbala na kuwazuia wasisonge mbele, Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa kibaraka wa mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya huko Kufa, alikabidhi jukumu la ukamanda wa jeshi la Yazid kwa Umar bin Saad.

Siku kama ya leo miaka 616 iliyopita, alizaliwa Ibn Khallouf mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga mkubwa wa Kiislamu.
Akiwa kijana mdogo alifanya safari mjini Makkah na baadaye Quds, Palestina huku akisafiri pia mjini Cairo, Misri baada ya kuwa ni kijana. Lengo la safari hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta elimu kiasi kwamba, akiwa na umri wa miaka 26 alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika vyuo vikubwa vya nchini Misri.
Mbali na hayo ni kwamba Khallouf alikuwa akisoma pia mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saw) na watu wa familia yake. Hadi leo turathi za msomi huyo zipo katika maktaba za Bairut, Lebanon na Damascus, Syria. *

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita John Boyd Dunlop raia wa Uingereza, alikuwa mvumbuzi wa kwanza wa gurudumu. Dunlop alifikia hatua ya kuvumbua gurudumu la magari baada ya utafiti wa miaka kadhaa. Alifariki dunia 1921.

Katika siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Julai mwaka 1899, alizaliwa mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway.
Kwa muda fulani Hemingway alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka kwa wepesi. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi.
Hemingway alipendelea sana kuwinda na alitumia muda mwingi katika shughuki hiyo. Alifariki dunia tarehe pili Julai 1961 baada ya kujipiga risasi na bunduki yake mwenyewe ya kuwindia, wakati akiisafisha. Hivyo, mkasa wa kifo cha baba yake ukawa umejirudia kwake baada ya kupita miaka 23.
Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni pamoja na kitabu cha "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na "For Whom The Bell Tolls".
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, kulifanyika maandamano makubwa mjini Tehran na kwenye miji mingine ya Iran baada ya Dakta Musaddiq kujiuzulu cheo cha Waziri Mkuu.
Wakati huo Ayatullah Kashani alitoa taarifa ya maneno makali baada ya Dakta Musaddiq aliyekuwa Waziri Mkuu kujizulu na Shah kumteuwa Ahmad Qavam mashuhuri kwa jina la Ghavam Sultaneh kuwa Waziri Mkuu.
Ayatullah Kashani alitoa taarifa hiyo akilalamikia vikali agizo la Shah la kumteuwa Ghavam kushika wadhifa huo. Ahmad Qavam ambaye alikuwa na uhusiano na wakoloni na kibaraka wa utawala wa kibeberu wa wakati huo, muda mfupi baada ya kuwa Waziri Mkuu, alianzisha njama za kutenganisha dini na siasa na kuendesha propaganda dhidi ya Ayatullah Kashani na wanaharakati wa Kiislamu nchini Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Julai 1954 ulitiwa saini mkataba wa kuacha vita kati ya Ufaransa na Vietnam na kukomesha ukoloni wa Ufaransa huko India na China mwishoni mwa mkutano wa Geneva.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kuanguka ngome imara ya Wafaransa iliyojulikana kwa jina la Dien Bien Phu nchini Vietnam Mei mwaka 1954. Makubaliano ya mkutano wa kimataifa wa Geneva, yalihudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Ufaransa, Marekani, Uingereza, China, Vietnam na Urusi ya zamani.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya kigeni vilipaswa kuondoka Vietnam, lakini Marekani kinyume na makubaliano ya Geneva, ikaamua kutuma majeshi katika eneo hilo kwa lengo la kuzuia kuungana maeneo mawili ya Vietnam ya kaskazini na ya kusini.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, meli ya kwanza ya biashara ya nyuklia iliyopewa jina la NS Savannah iliwekwa majini huko Marekani.
Baada ya kugunduliwa atomu na wasomi kutambua nguvu kubwa na nishati ya atomiki, ilijitokeza fikra ya kutumia nishati hiyo katika masuala mbalimbali. Hata hivyo inasikitisha kwamba, nishati hiyo ilitumiwa kwa mara ya kwanza kielimu katika kutengeneza mabomu ya nyuklia. Suala hilo lilichochea mashindano ya kutengeneza silaha na mabomu ya nyuklia kati ya madola makubwa na kuiweka dunia katika ncha ya vita vya nyuklia.
Meli ya NS Savannah ilikuwa matokeo ya jitihada za wasomi za kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 21 Julai mwaka 1958 meli hiyo ya kibiashara iliyokuwa ikitumia nishati hiyo iliwekwa majini na kuanza kufanya kazi. NS Savannah ilikuwa meli ya kwanza iliyotumia nishati ya nyuklia kuvuka habari ya Atlantic.