Jul 26, 2023 02:10 UTC
  • Leo katika Historia, Jumanne Julai 25

Leo ni Jumanne tarehe 7 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hjria sawa na Julai 25 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, Omar Bin Saad, alitoa amri ya kuuzuia msafara wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) kutumia kwa aina yoyote maji ya mto wa Furati (Euphrates.) Baada ya Ubaidullah Bin Ziyad, kutuma jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana vita na mjukuu huyo wa Mtume, alituma barua kwa Ibn Saad ili kumzingira Imam Hussein na masahaba zake. Katika ujumbe huo, Bin Ziyad alimtaka Omar Bin Saad kumwamuru Imam Hussein kumtambua rasmi na kumpa mkono wa utiifu Yazid mwana wa Muawiya. Sehemu nyingine ya barua hiyo ilimtaka kamanda huyo wa jeshi katili kumtenga mjukuu huyo wa Mtume wa Allah na maji ya Mto Furati na asimruhusu kamwe kunywa maji ya mto huo yeye au vamilia yake. Bila kuchelewa Ibn Saad aliwaamuru askari 500 wapanda farasi kumzuia Imam Hussein na maji ya mto huo. Kitendo hicho cha kikatili, kilijiri ikiwa ni siku tatu kabla ya kuuawa shahidi Imam Huusein (as). Hata hivyo Abul-fadhlil-Abbas alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwaletea maji watu wa msafara huo ingawa hata hivyo askari wale katili walimzuia na kumuua kinyama mtukufu huyo. Hadi asubuhi ya siku ya tisa ya mwezi huu wa Muharram, hakukuwa na tone la maji lililokuwa limesalia kwa wafuasi wa mjukuu huyo wa Mtume (Imam Hussein) suala ambalo liliwafanya watukufu hao kuvumilia tabu ya kiu kali kutokana na joto kali lililokuwepo eneo hilo.

Mto Furati

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, alizaliwa Sayyid Mohammad Hadi Milani, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia. Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammad Hadi Milani alizaliwa tarehe saba mwezi Muharram mwaka 1313 Hijiria Qamaria huko mjini Najaf, Iraq. Alianza kusoma elimu ya dini akiwa na umri mdogo ikiwa ni pamoja na kujifunza Qur'ani Tukufu mjini hapo. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kifarsi na Kiarabu huku akiandika pia vitabu vingi. Aidha kando na shughuli hiyo alikuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi elimu ya hawza ya kidini na kufikia daraja ya umarjaa. Msomi huyo alitambulika kwa uchaji-Mungu, taqwa, na tabia njema ya hali ya juu. Kitabu cha 'Muhaadharat fii Fiqhil-Imaamiyyah' ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammad Hadi Milani

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina. Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China. Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa.   

Katika siku kama ya leo miaka 845 iliyopita, Wapalestina 62 wasio na hatia  waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina. Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina. 

Jinai za Wazayuni 

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani. Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadaye alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na fikra za kisiasa. Miongoni wma vitabu vya msomi huyo ni Uislamu na Usoshalisti na Fikra za Kisiasa za Magharibi. 

Dakta Hamid Inayat

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga na baharini huko kusini mwa Lebanon. Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.