Jul 30, 2023 22:58 UTC
  • Jumatatu, Julai 31, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria, sawa na 31 Julai 2023 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, yaani sawa na tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa wazi wazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wacha-Mungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abdullah bin Afif usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkatakata kwa mapanga. 

Tarehe 31 Julai miaka 217 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza. Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya Bahari za Atlantic na Hindi. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa. 

Miaka 137 iliyopita aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa Hungary. Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Nyimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt.   

Franz Liszt

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwanaanga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka. Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta. Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na mabaki ya mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwao ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight." 

Antoine de Saint-Exupery

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita kiongozi wa Waislamu weusi wa Marekani, Elijah Muhammad alitoa wito wa kuundwa dola la watu weusi nchini Marekani chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya nchi hiyo. Lengo la kutolewa fikra hiyo lilikuwa kukomboa Wamarekani weusi kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa kimbari na kizazi nchini Marekani. Elijah Muhammad mwenyewe ambaye aliathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani kwa jina la la Wallace Fard Muhammad na kuwa Muislamu, alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na taathira kubwa katika harakati hiyo ya kudai dola la Wamarekani weusi. Elija Muhammad aliasisi chama cha Umma wa Uislamu (Nation of Islam) na kujenga misikiti na vituo kadhaa kwa ajili ya Waislamu wa Marekani. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa harakati hiyo ya Waislamu weusi wa Marekani kama Malcolm X walikataa na kupinga baadhi ya itikadi za kidini na siasa za Elijah Muhammad. 

Elijah Muhammad

Tarehe 9 Mordad mwaka 1366 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 36 iliyopita kulitokea tukio la kusikitisha la Ijumaa ya Damu mjini Makka. Siku hiyo mamia ya mahujaji wa Kiirani na mahujaji kadhaa wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Siku hiyo askari wa Kiwahabi wa Saudia walishambulia mahujaji hao kwa risasi na kuua mahujaji 400 za Kiirani na kujeruhi wengine zaidi ya elfu moja.