Jul 31, 2023 23:31 UTC
  • Jumanne, tarehe Mosi Agosti, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 14 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Agosti 2023.

Siku kama ya leo miaka 182 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, moja ya miji maarufu ya Iran, Sayyid Sadruddin Musawi Amili, msomi na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Sayyid Sadruddin Musawi Amili alizaliwa katika moja ya viunga vya mji wa Jabal Amel, nchini Lebanon. Akiwa kijana mdogo alisafiri nchini Iraq ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika hawza ya elimu ya mjini Najaf, alianza kufanya utafiti katika elimu kadhaa kama vile fiqhi, usulul fiqhi na Hadithi na kufikia daraja la juu katika uwanja huo. Sayyid Sadruddin Musawi Amili ameandika vitabu mbalimbali katika uga wa elimu ya sheria, nahawu na mifano ya aya za Qur’an Tukufu.

Sayyid Sadruddin Musawi Amili

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Abul Qasim Lahori. Abul Qasim Bin Hussein Bin Naqi Ridhawi Taqawi Lahori na aliyekuwa faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu alizaliwa Kashmir. Aalikuwa miongoni mwa maulama wakubwa nchini India na ameandika vitabu vingi. 

Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na 'Burhanu Shaqqul-Qamar wa Raddun-Nayril-Akbar' 'As-Siratul-Mustaqim.'

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Benin ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa. Wafaransa walianza kuingilia masuala ya kisiasa na kiuchumi ya Benin katika nusu ya pili ya karne ya 19 na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo mwaka 1892. Ufaransa iliendelea kuikoloni Benin hadi mwaka 1958 na hatimaye mwaka 1960 katika siku kama ya leo nchi hiyo kajipatia uhuru. 

Katika siku kama ya leo mika 48 iliyopita, mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo hasa kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979.

Miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Aal-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.

Mfalme Fahd

Tarehe Mosi Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama. Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika mji wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama. Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mama.