Aug 04, 2023 00:47 UTC
  • Ijumaa tarehe 4 Agosti, 2023

Leo ni Ijumaa mwezi 17 Muharram 1445 Hijria sawa na Agosti 4 mwaka 2023.

Katika siku kama hii ya leo miaka 547 iliyopita Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa zaidi wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria alifariki dunia katika mji wa Harat katika Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Silsilatu al Dhahab", Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharestan." 

Siku kama ya leo miaka 492 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni Jame Abbasi na Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrihul Aflak na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan, Iran. 

Sheikh Bahai

Miaka 231 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na Mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania.   

Percy Bysshe Shelley

Miaka 218 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland alizaliwa.  Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton taratibu akaanza kuwa na mapenzi makubwa na elimu za fizikia na hisabati. Aidha alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari ni mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865.   

William Rowan Hamilton

Katika siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark. Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo. Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo.   

Hans Christian Andersen

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki.   

Mustafa Kemal Ataturk na Reza Shah

Katika siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, alizaliwa katika mji wa Mash'had, Iran, Ayatullah Sayyid Ali Sistani faqihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kishia.  Alianza kujifunza Qur'ani akiwa na miaka 5,na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf, Iraq hapo baadaye. Hii leo Ayatullah Ali Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali amekuwa pia na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu.   

Ayatullah Sayyid Ali Sistani

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye Bahari ya China ya Kusini. Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini. 

Vita vya Vietnam