Leo katika Historia, Ijumaa tarehe 18 Agosti 2023
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Safar 1445 Hijria sawa na Agosti 18 mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya serikali yake.
Tarehe Mosi Safar miaka 1384 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq.

Siku kama ya leo miaka 1370 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.
Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji.
Katika siku kama hii ya miaka 44 iliyopiya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuvunjwa mzingiro na kukombolewa eneo la mpakani la Paveh huko Magharibi mwa Iran. Eneo hilo lilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na baadhi ya makundi yaliyokuwa yakipiga vita Mapinduzi ya Kiislamu. Makundi hayo yalikuwa yakisaidiwa na madola ya kigeni na yalianzisha machafuko katika maeneo mbalimbali ya Iran baada tu ya ushindi wa Mapindzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya amri hiyo ya Imam Khomeini wananchi na wanajeshi waliharakia kwenda eneo la Paveh na kulikomboa kikamilivu.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.
Na katika siku kama hii ya leo miaka 15 ilioyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliungana na kundi la nchi 10 zenye teknolojia ya kurusha chombo cha kkuupeleka angani satelaiti kilichopewa jina la Safire omid kwa maana ya Balozi wa matumaini. Operesheni hiyo ilifanyika wka mabafanikio.
