Jumapili, 20 Agosti, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 3 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria mwafaka na tarehe 20 Agosti 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1388 iliyopita yaani Mwezi 3 Safar mwaka 57 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, alizaliwa katika mji wa Madina, Imam Muhammad Baqir (AS), mjukuu kipenzi wa Bwana Mtume SAW na Imamu wa Tano wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Ukamilifu wa kimaanawi na kielimu ambayo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu waliyotunukiwa Ahlubayti wa Mtume SAW, ulidhihirika kwa uwazi katika shakhsia ya Imam Muhammad Baqir (AS) pia. Katika kipindi cha miaka 19 ya Uimamu wa mtukufu huyo, ambacho kilisadifiana na miaka ya mwishoni ya utawala wa Bani Umayyah, yalipatikana mazingira mwafaka katika jamii kwa yeye kuweza kuimarisha misingi ya kifikra na kiutamaduni ya Waislamu. Fani nyingi za elimu zilistawishwa na kuenea katika jamii ya Waislamu kupitia chuo cha fikra cha mtukufu huyo pamoja na mwanawe, yaani Imam Jaafar Sadiq (AS); na hata wanafunzi wake walikuja kuwa wavumbuzi wa fani mbalimbali mpya za elimu. Lakini sambamba na hayo, Imam Baqir hakughafilika pia na kupambana na dhulma na uonevu wa utawala wa kijabari wa Bani Umayyah na ndiyo maana katika mwaka 114 Hijria Qamaria aliuliwa shahidi na mtawala wa zama hizo. Tunachukua fursa hii pia kukupeni mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa mjukuu huyo kipenzi wa Mtume SAW. ***
Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, mji mkuu wa Ubelgiji Brussels ulidhibitiwa na vikosi vya Ujerumani. Huu ulikuwa mji mkuu wa kwanza kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani wakati wa kujiri vita vikuu vya kwanza vya dunia. ***

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiria ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988. Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani, USS Vincennes, ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu 298 waliokuwemo. Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa. ***

Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii. ***

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, aliaga dunia Muhammad Hussein Behjati, mshairi na mwanazuoni mahiri wa Kiirani. Alizaliwa 1314 Hijria Shamsia. Muhammad Hussein Behjati alianza kujihusisha na masomo tangu akiwa na umri wa miaka 7. Mwaka 1331 alielekea katika mji wa Qum. Msomi huyo aliposoma pamoja na Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mas'ud Khomeini na Ayatullah Khamenei. Alikuwa pia mmoja wa wanafunzi wa Imam Khomeini na Ayatullah Burujerdi. ***
