Nov 25, 2023 04:33 UTC
  • Jumamosi, 25 Novemba, 2023

Leo ni Jumamosi 11 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 25 Novemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1063 iliyopita alifariki dunia Ali bin Isa Rumani, mtaalamu mkubwa wa elimu ya nahwu na fasihi ya Kiarabu. Bin Issa mbali na kutabahari katika elimu ya fasihi ya Kiarabu, alikuwa pia mtaalamu wa elimu za fiqhi, teolojia, na Qur’ani. Miongoni mwa vitabu muhimu vilivyoandikwa na Ali bin Isa Rumani ni kile cha ‘I’jaazul-Qur’an’. ***

Ali bin Isa Rumani

 

Siku kama ya leo miaka 848 iliyopita, alizaliwa Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tusi, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na mwanaye na kuasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe. Kituo hicho kiliasisiwa mwaka 657 Hijria, huko kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naasiri’, ‘Awswaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat. ***

Nasiruddin Tusi

 

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na  Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa. Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo. Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba. ***

Charles Luis Alphonse Laveran

 

Miaka 73 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 4 Azar mwaka 1329 Hijiria Shamsia, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta huko kusini mwa Iran. Vilevile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa ni tishio kwa maslahi ya taifa. ***

Kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa

 

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 Muhammad Hadi Farzaneh, maarufu kwa jina la Hakim Farzaneh, mtaalamu mkubwa wa elimu ya theolojia na falsafa. Hakim Farzaneh alizaliwa mwaka 1302 Hijiria katika moja ya maeneo ya mji wa Isfahan. Alisoma elimu ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea mjini Isfahan kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo alipata kusomea elimu mbalimbali muhimu hususan theolojia na falsafa. Aliweza kuinukia kielimu na kuwa msomi mkubwa kiasi kwamba mwishoni mwa umri wake alikuwa miongoni mwa wataalamu wa taaluma hizo. Baadaye alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji hadi alipofariki dunia. ***

Muhammad Hadi Farzaneh

 

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya uwagaji damu. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji. ***

Jenerali Mobutu Sese Seko

 

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 4 Azar 1345 Hijria Shamsia, alifariki dunia mhadhiri wa chuo kikuu Jabbar Baghche Ban baada ya kutumia muda wake mwingi katika kuwahudumia kwa moyo mkunjufu viziwi wa Iran. Mnamo mwaka 1302 Hijria Shamsia, Baghche Ban alianzisha kituo cha kuwafunza na kuwalea watoto viziwi katika mji wa Tabriz, ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na huo ndio uliokuwa mwanzo wa jitihada za muda mrefu za mhadhiri huyo za kuwafundisha watoto viziwi. Aliwafundisha watoto hao kusoma na kuandika kwa kugundua mbinu mpya za kujifunza alfabeti ambayo inatumika siku hizi. Baghche Ban pia mwaka 1313 Hijiria Shamsia alianzisha shule ya kwanza ya wanafunzi viziwi nchini Iran. ***

Jabbar Baghche Ban

 

Miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi. Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic. ***

Bendera ya nchi ya Suriname

 

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita alifariki dunia Vasiliy Ivanovich Alekseyev, bingwa mnyanyuaji uzani wa nchini Russia na kimataifa. Alekseyev alipata ushindi mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani na mwaka 1976 Montréa, Canada kwa kujinyakulia medali za dhahabu. Katika kipindi cha ushindi wake, Vasiliy Ivanovich Alekseyev aliweka rekodi ya dunia. Yeye alikuwa mnyanyuaji uzani ambaye aliweza kuweka rekodi ya kunyanyua kilogramu 645 kwa kupindukia kilogramu 600. Mwaka 1993 Shirikisho la wanyanyuaji uzani duniani lilimteua Alekseyev kuwa mmoja wa mabingwa wakubwa katika fani hiyo. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 nchini Ujerumani kutokana na matatizo ya moyo. ***

Vasiliy Ivanovich Alekseyev

 

 

Tags