Dec 13, 2023 02:39 UTC
  • Tuujue Uislamu (1)

Assalaam Alaykum Wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya.

Karibuni katika kipindi hiki kipya cha "Tuujue Uislamu" kipindi ambacho kitakuwa kikikujieni kila juma badala ya kipindi cha Mchango wa Maulamaa wa Kiiislamu Katika Uislamu ambacho mfululizo wake ulimalizika juma lililopita. Sehemu ya kwanza ya kipindi hiki itaeleza malengo ya kipindi hiki pamoja na umuhimu na nafasi ya dini katika katika maisha ya mwanadamu. Jiungeni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache.Wapenzi wasikilizaji katiika mfululizo wa kipindi hiki kipya cha Tuujue Uislamu tunakusudia kuelezea kwa lugha nyepesi kuhusu Misingi ya Dini ya Uislamu pamoja na mafundisho yake.

Kama mnavyojua hii leo mwanadamu anahitaji kuwa na udiriki na ufahamu sahihi kumhusu yeye pamoja na ulimwengu kwa ujumla. Kutokana na kuibuka vita na matukio machungu na ya kuogopesha katika karne ya Miladia, kumekuwa na taswira tata na ya kukakatisha tamaa kwa akthari ya walimwengu kuhusiana na mustakabali wa dunia. Pamoja na hayo hitajio la ndani la mwanadamu wa leo la kupata kimbilio la uhakika ambalo litamfanya awe na mtazamo chanya na mzuri kuhusiana na mustakabali na ambalo litakidhi mahitaji yake linahisika zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Katika mfululizo wa vipindi hivi, tutajaribu kumjuza na kumfahamisha msikilizaji kuhusiana na Uislamu na mipango yake ikiwa ndio dini ya mwisho na kamili zaidi ya Mwenyezi Mungu na ambayo alikuja nayo mbora wa viumbe Mtume Muhammad (saww).

Aidha katika mfululizo huu wa "Tuujue Uislamu" tutajadili na kutathmini maudhui ya Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu athari na faida zake, falsafa na malengo ya kutumwa Mitume kwa mtazamo wa Uislamu.

 Tutatupia jicho pia maudhui zingine kama uadilifu wa Mwenyezi Mungu, ufufuo na Uimamu maudhui ambazo ni katika Usul Din yaani Misingi ya Dini. Aidha kuhusiana na Furu' al-Din (Matawi ya Dini) tutajadili maudhui kama Swala, Saumu, Hija na Jihadi.

Lakini kabla ya kuingia katika maudhui, kuna ulazima wa kutoa utangulizi na kuzungumzia umuhimu na nafasi ya dini katika maisha ya mwanadamu na jamii kwa ujumla kukumbusha nukta kadhaa.

*********

Moja ya maswali ya kimsingi ya mwanadamu ni nini faida na nafasi ya dini katika maisha yake? Kwa nini ni lazima kuwa na kidini na inawezekana kuishi bila dini? Historia inaonyesha ukweli huu kwamba, tangu kuumbwa kwake, mwanadamu huyu amekuwa na mwelekeo wa kina na wenye mizizi wa kuabudu na kuwa na dini. Dini ni moja ya adia na zawadi kuu za Mwenyezi Mungu na hisia ya kuabudu daima imekuwa pamoja na wanadamu popote awapo. Kwa mujibu wa ushahidi na nyaraka za historia, kwa namna fulani karibu jamii zote za wanadamu zimekuwa na mwelekeo wa kidini. Hili lenyewe linaonyesha kwamba, dini ni hitajio kuu na asili na lililofichika ndani na katika uwepo wa mwanadamu. Kwa msingi huo, daima mwanadamu ni mwenye kuhitajia dini na mafundisho yake na kamwe hakuna wakati ambao utawadia na mwanadamu akawa si mwenye kuhitajia tena dini.

Ernest Renan, mwanafalsafa Mfaransa na mtaalamu wa mambo ya nchi za Mashariki anasema kuhusiana na taathira za mwanadamu kushikamana na dini kwamba:  Yumkini siku moja kila kitu ninachokipenda kinaweza kuharibiwa na kusambaratika, na kila kitu ambacho ni burudani na ladha kwangu kikaangamizwa; lakini ni muhali mapenzi na huba ya dini ikatoweka na kufutika. Bali, itabaki daima na katika nchi yangu, na uwepo wangu utakuwa shahidi wa kweli na wa wazi wa kubatilika umaada.

Kwa mtazamo wa Will Durant mwanahistoria na mwandishi wa Kimarekani ni kuwa, dini ni roho ya maisha. Durant anaema: Maisha bila dini yanachosha, hukosa msukumo na huwa mithili ya mwili usio na roho.

Tukirejea katika Qur'ani, tunaona Mwenyezi Mungu anachora ramani ya njia kuhusiana na muelekeo wa mwanadamu katika dini na kulitaja hilo kuwa, ni jambo la kifitra na kimaumbile na hitajio la mwanadamu. Aya ya 30 ya Surat al-Rum inasema:

Basi na uelekeze uso wako sawasawa kwenye dini-ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliiko katika umbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndio dini ya sawasawa, lakini watu wengi hawajui.

Allama Muhammad Hussein Tabatabai, mwanafalsafa na msomi mkubwa Kishia na mfasiri wa Tafsiri ya al-Mizan anasisitiza nukta hii kwamba, ratiba ya maisha ya mwanadamu inapasa kwenda sambamba na fitra na maumbile yake aliyoumbwa nayo na yenye mtazamo jumuishi.

Mwenyezi Mungu mjuzi na mwenye hekima na busara alimuumba mwanadamu na kuweka ndani yake kila aina ya mahitaji, vipaji na hamu ya kuelekea katika ukamilifu. Ili mwanadamu aweze kufikia katika mafanikio na saada ya milele ni lazima achague njia sahihi na ya uhakika ya kuishi. Lakini kwa sababu kuna vikwazo vingi, hatari, upotofu na mambo ya kupotosha mbele yake, kuchagua njia sahihi si rahisi. Hapa, hekima ya Mungu inahukumu kwamba asimwache mwanadamu peke yake na hivyo amuonyeshe njia ya kufikia hatima na malengo yake na kukuza vipawa na nguvu zake za ndani kupitia ufunuo. Hii ni sababu mojawapo ya mwanadamu kuhitajia dini. Mwanafikra Shahidi Ustadh Murtadha Mutahhari anaandika kuhusu madhumuni ya kuja na kutumwa Mitume ambao ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu na wabebaji wa ujumbe na risala ya dini kwa ajili ya wanadamu kwamba:

Nabii ni njia na wenzo wa mawasiliano kati ya wanadamu na ulimwengu mwingine na kwa hakika ni daraja kati ya wanadamu na ulimwengu wa ghaibu.

Ayatullah Nasser Makarem Shirazi, mwanafikra na mfasiri wa Qur'ani, akieleza ulazima wa dini kwa wanadamu, anaona kuwa ni kinga kwa ajili ya misingi ya juu ya kimaadili na anaandika kuhusiana na hili: Dini ni harakati ya pande zote kwa ajili ya watu. kurekebisha mawazo na imani, kukuza misingi ya juu ya kimaadili, mahusiano bora ya watu katika jamii na kuondoa ubaguzi wowote katika mwanga wa imani kwa Mwenyezi Mungu na hisia ya ndani ya uwajibikaji.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Msikose kujiunga nami katika sehemu ya pili ya kipindi hiki cha "Tuujue Uislamu" ambapo tutaendelea kujadili umuhimu na udharura wa kuweko dini katika maisha ya mwanadamu. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakienii kila la kheri.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh