Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi la wanamgambo wenye silaha, Burkina Faso
Makumi ya wanajeshi na raia wameuawa katika mashambulizi mawili yaliyofanyika kaskazini mashariki mwa Burkina Faso mapema wiki hii ambayo yalitekelezwa na wanamgambo wenye silaha.
Chanzo kimoja cha usalama kimesema shambulio "kubwa" lilitekelezwa siku ya Jumatatu likilenga kitengo cha jeshi katika kijiji cha Dargo. Chanzo hicho kimesema hujuma hiyo ilifanywa na "makundi ya kigaidi yenye silaha," na kupelekea kuuawa "makumi ya watu baina ya upande mbili."
Chanzo kingine cha usalama kimeripoti kwamba wanamgambo hao walifanya shambulio la pili siku hiyo hiyo dhidi ya msafara wa misaada kwenye barabara inayounganisha miji ya Dori na Gorom-Gorom.
Askari na raia waliuawa katika shambulizi hilo, haswa madereva wa malori yalikuwa yamebeba vifaa.
Meneja wa kampuni ya kusafirisha mizigo ya nchi kavu amethibitisha kuwa msafara huo ulishambuliwa, akisema kuwa "madereva wapatao 20 na wanafunzi wao wameuawa."
Kundi moja lenye uhusiano na al-Qaeda ambalo pia linafanya harakati katika nchi za Mali na Niger limetangaza kuhusika na hujuma hiyo.
Burkina Faso, ambayo karibu asilimia 40 ya ardhi yake inadhibitiwa na wanamgambo wenye silaha, imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya kundi hilo la Daesh tangu mwaka 2015.