Utafiti: Zaidi ya watoto milioni 12 kufariki dunia ifikapo 2045
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134068-utafiti_zaidi_ya_watoto_milioni_12_kufariki_dunia_ifikapo_2045
Utafiti mpya uliotolewa na Taasisi ya Gates Foundation unaonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza katika karne hii, idadi ya watoto duniani wanaofariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano baada ya kuzaliwa inatarajiwa kuongezeka.
(last modified 2025-12-08T10:23:56+00:00 )
Dec 08, 2025 10:23 UTC
  • Utafiti: Zaidi ya watoto milioni 12 wa chini ya umri wa miaka 5 kufariki dunia ifikapo 2045
    Utafiti: Zaidi ya watoto milioni 12 wa chini ya umri wa miaka 5 kufariki dunia ifikapo 2045

Utafiti mpya uliotolewa na Taasisi ya Gates Foundation unaonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza katika karne hii, idadi ya watoto duniani wanaofariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano baada ya kuzaliwa inatarajiwa kuongezeka.

Watafiti wa taasisi hiyo wanataja sababu kuu kuwa ni kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha misaada ya maendeleo ya kimataifa kutoka nchi kadhaa.

Sehemu moja ya ripoti yao inasema, ikiwa upunguzwaji wa ufadhili kwa asilimia 20 utaendelea, watoto milioni 12 zaidi walio chini ya umri wa miaka 5 wanaweza kupoteza maisha ifikapo mwaka wa 2045.

“Kwa miaka 25 iliyopita tumepiga hatua kubwa katika sekta ya afya kimataifa, hasa kwa watoto,” alisema Margaret Miller, afisa mwandamizi wa programu katika Taasisi ya Gates Foundation. “Ni jambo la kusikitisha sana kwamba mafanikio hayo sasa yako hatarini.”

Maendeleo ya kisayansi na kijamii katika miongo ya hivi karibuni yamesababisha vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kupungua kwa takriban watoto 88 kwa kila 1,000 wanaozaliwa hai tangu mwaka wa 1990 hadi watoto 36 mwaka 2020.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka mwaka huu hadi 37, kulingana na ripoti ya Wakfu wa Gates iliyochapishwa wiki iliyopita ikiwa ni mara ya kwanza karne hii vifo vya watoto vimeongezeka.

Mwaka jana, takriban watoto milioni 4.6 walikufa kabla ya kutimiza miaka 5; mwaka huu, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya vifo 200,000.