Serikali ya Tanzania yawataka wananchi wasiokuwa na dharura kubaki nyumbani Disemba 9
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134072-serikali_ya_tanzania_yawataka_wananchi_wasiokuwa_na_dharura_kubaki_nyumbani_disemba_9
Serikali ya Tanzania imewataka wananchi kusalia majumbani kesho Desemba 9, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Uhuru wa Tanganyika.
(last modified 2025-12-08T10:43:22+00:00 )
Dec 08, 2025 10:43 UTC
  • Wananchi wa Tanzania watakiwa kubakia majumbani kesho Disemba 9
    Wananchi wa Tanzania watakiwa kubakia majumbani kesho Disemba 9

Serikali ya Tanzania imewataka wananchi kusalia majumbani kesho Desemba 9, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Uhuru wa Tanganyika.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kufuatia kuibuka kwa taarifa za wito wa maandamano unaosambaa kupitia mitandao ya kijamii, hatua iliyoifanya serikali kuongeza tahadhari kuelekea siku hiyo muhimu ya kitaifa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, licha ya umuhimu wa siku ya Uhuru katika historia ya taifa, ni busara kwa wananchi kutumia siku hiyo kwa utulivu, hususan kwa wale wasiokuwa na dharura.

Hatua hiyo imekuja wakati ambapo tayari serikali imesitisha shughuli za sherehe za kitaifa za mwaka huu. Awali, ilitangazwa kuwa fedha zilizopangwa kwa ajili ya maadhimisho ya Uhuru zingeelekezwa katika ukarabati wa miundombinu iliyoathiriwa vibaya na vurugu za siku tatu zilizotokea kuanzia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa takwimu za awali zilizotolewa na serikali, jumla ya ofisi za serikali 756 ziliharibiwa, vituo vya mabasi ya mwendo kasi 27, huku mabasi 6 yakiteketezwa kwa moto.

Nyumba binafsi 273, vituo vya polisi 159, na vituo binafsi vya mafuta 672 navyo vilipigwa au kuchomwa moto. Aidha, zaidi ya magari binafsi 1,642 yaliteketezwa, pikipiki 2,268, pamoja na magari ya serikali 976, yakitajwa kuwa miongoni mwa mali zilizoathirika katika machafuko hayo.

Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano yoyote yaliyopangwa kufanyika kesho Disemba 9.

Akizungumza na vyombo vya habari leo, Waziri wa mambo ya ndani, George Simbachawene amesema maandamano hayo ni haramu kwa kuwa hayana kibali kwa mujibu wa sheria, hayajulikani nani anayandaa, hayana ujumbe mahususi na hayana ukomo ili jeshi la polisi liweze kutoa huduma ya kuyalinda.