Mapigano yaendelea: Makubaliano ya amani ya DRC na Rwanda yabakia kuwa ndoto
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134076-mapigano_yaendelea_makubaliano_ya_amani_ya_drc_na_rwanda_yabakia_kuwa_ndoto
Mapigano makali yameendelea kujiri Uvira mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakikabiliana na jeshi la Kongo linaloungwa mkono na wanajeshi wa Burundi.
(last modified 2025-12-08T11:05:16+00:00 )
Dec 08, 2025 11:05 UTC
  • Mapigano yaendelea: Makubaliano ya amani ya DRC na Rwanda yabakia kuwa ndoto
    Mapigano yaendelea: Makubaliano ya amani ya DRC na Rwanda yabakia kuwa ndoto

Mapigano makali yameendelea kujiri Uvira mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakikabiliana na jeshi la Kongo linaloungwa mkono na wanajeshi wa Burundi.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa raia wapatao 20 wakiwemo watoto wamejeruhiwa. Aidha, takriban wanajeshi 20 wa Burundi wameripotiwa kuuawa kwenye mapigano hayo tangu yalipozuka upya Jumatatu iliyopita. Hata hivyo, vyanzo kadhaa vya kijeshi vimeeleza kuwa kwa sasa  wanajeshi wa Burundi  wamewadhibiti waasi wa M23 na kuwasababishia pia hasara.

Duru za serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimetangaza kuwa, waasi wa M23, wakisaidiwa na jeshi la Rwanda wanaendelea kusonga mbele kuelekea eneo la Kivu Kusini. Maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao huku mapigano yakizidi kupamba moto.

Hayo yanajiri siku chache tu tangu marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda waliposaini makubaliano ya amani mjini Washington, Marekani mbele ya rais wa nchi hiyo Donald Trump, yaliyoelezewa na ikulu ya nchi hiyo kuwa ni ya "kihistoria".

Marais Félix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda walisafiri hadi mji mkuu huo wa Marekani kwa ajili ya utiaji saini huo, ambapo waliungana na viongozi kutoka mataifa mengine kadhaa ya Afrika.

Makubaliano hayo yanaifungulia njia serikali ya Marekani na makampuni ya nchi hiyo kuchota madini adimu na yenye umuhimu mkubwa yaliyoko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.