Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Azerbaijan zaazimia kuimarisha zaidi ushirikiano
-
Mazungumzo ya Rais wa Azerbaijan na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alielekea Baku kushauriana na maafisa wakuu wa Jamhuri ya Azerbaijan leo asubuhi amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Ilham Aliyev.
Katika mkutano huo, masuala mbalimbali ya pande mbili yalijadiliwa, ikiwa ni pamoja na mchakato wa mwingiliano wa kisiasa, masuala yanayohusiana na ujirani, na taratibu za kusimamia na kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa wa Iran amewasilisha salamu za dhati za Rais Masoud Pezeshkian kwa Rais wa Azerbaijan.
Akiashiria uhusiano mkongwe na wa kina baina ya mataifa hayo mawili, Araqchi amesisitiza azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuimarisha na kupanua uhusiano na Jamhuri ya Azerbaijan katika nyanja zote zenye maslahi kwa pande zote mbili.
Akiashiria umuhimu wa mtazamo wa muda mrefu katika mahusiano ya ujirani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesitiza jukumu la mashauriano ya kidiplomasia endelevu ili kutatua suutafahamu na kusimamia masuala ya pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan wakati akitoa salamu kwa Rais Pezeshkian ameeleza kuwa ziara ya Rais Pezeshkian Baku ilikuwa ya kihistoria na imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha maelewano na kuboresha uhusiano kati ya Baku na Tehran.
Akielezea furaha yake juu ya mwelekeo unaokua wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Rais Ilham Aliyev alisisitiza utayari wa Azerbaijan kutumia uwezo wote uliopo kupanua uhusiano.
Katika kikao hiki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alielezea mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na matukio ya kieneo.