Dec 13, 2023 02:45 UTC
  • Tuujue Uislamu (2)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu ya pili ya kipindi hiki kipya cha Tuujue Uislamu.

Katika sehemu ya kwanza ya kipindi hiki tuliashiria malengo jumla ya kipindi hiki na maudhui tutakazozitupia jicho na kuzibainisha katika mfululizo huu. Aidha tuligusia kwa mukhtasari katika sehemu ya kwanza ya kipindi hiki kwamba, dini ni hitajio kuu na asili na lililofichika ndani na katika uwepo wa mwanadamu. Kwa msingi huo, daima mwanadamu ni mwenye kuhitajia dini na mafundisho yake na kamwe hakuna wakati ambao utawadia na mwanadamu akawa si mwenye kuhitajia tena dini. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa pamoja nami katika dakika hizi chache za kipindi hiki cha Tuujue Uislamu, hii ikiwa na sehemu ya pili ya mfululizo huu.

Kwa kuzingatia kwamba, kushikamana na dini au kuwa mtu wa dini ni muelekeo wa kimaumbile, kuna wakati wanadamu hughafilika na jambo hilo, hivyo Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume waliokuja na risala na Wahyi ili waje kuizindua na kuiamsha fitra hii ya mwanadamu na kumtaka mwanadamu asikilize kwa makini mwito wake wa ndani. Baada ya Mitume wa Allah kuja, kwa amri ya Muumba waliwafundisha wanadamu mafundisho mbalimbali, wakatoa miongozo, sheria, maadili mema n.k ambapo moja ya mafundisho hayo ni kumfanya mwanadamu awe na ufahamu na udiriki sahihi wa maisha.

Kimsingi ni kuwa, moja ya utendaji wa kimsingi wa dini ni kubainisha fasili, maana na mafuhumu ya maisha. Kila mwanadamu hujuuliza: Maisha au kuishi ni kwa ajili ya nini? Taabu, mashaka na machungu katika ulimwengu huu yana maana gani? Na kiuujumla hivi dunia ina thamani ya kuishi ndani yake au la?

Aina ya majibu ya maswali haya yanaainisha muelekeo na malengo ya kuishi hapa duniani. Ikiwa mwanadamu huyu hatapata majibu ya kimantiki na yenye kukubalika ya maswali haya atakumbwa na kutumbukia katika mambo yasiyo na maaana, ambayo hayana malengo na hivyo atakuwa ni mwenye kutangatanga na yumkini akaingia katika maktaba na njia za kifikra zisizo sahihi. Katika mazingira kama haya, itikadi yoyote ya hurafa na potofu yumkini ikaingia na kupenya katika roho yake na daima huathiri mawazo na fikra zake.

Mwelekeo wa mwanadamu katika aina yoyote ya upotofu ambayo huko nyuma imewahi kushuhudiwa pia hata kwa wasomi, chimbuko lake ni ombwe hili la kiroho.

Dini inajaza ufa na ombwe hili la kifikra na kiaidiolojia kwa mafundisho sahihi na ya kimantiki na inamzuia mwanadamu huyu asielekee katika mambo ya batili na upuuzi. Dini humwezesha mwanadamu kuwa na malengo ya juu na yenye thamani na kumsaidia kufikia malengo hayo. Nafasi ya dini katika maisha ya mwanadamu ni sawa na jukumu la dira katika meli.  Kwa maana kwamba, katika bahari ya maisha yenye misukosuko, dini huonyesha mwelekeo sahihi na njia ya kufika katika ufukwe wa wokovu. Dini hutoa ufafanuzi maalumu wa uhusiano kati ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu na inamuonyesha mwanadamu kituo cha mwanzo na cha mwisho. Hata hivyo ni jambo lisilo na shaka ni kwamba, kuwa na kitu hiki kulazimu kuwa na picha na taswira ya wazi ya mfumo wa ulimwengu. Mtu wa dini anaweza kufikia taswira ya kimantiki na inayokubalika kiakili ya mfumo wa ulimwengu kwa msaada wa akili na ufunuo yaani Wahyi.

Carl Gustav Jung, mtaalamu wa magonjwa ya akili na mwanafikra wa Uswisi, anaandika kuhusu umuhimu wa maana ya maisha kwamba: Miongoni mwa wagonjwa ambao nimekutana nao katika nusu ya pili ya maisha yangu, tatizo lao wote mwisho wa siku lilikuwa likihusiana na kutafuta mtazamo kuelekea maisha. Inawezekana kusema kwa uhakika kabisa kwamba, wote hao walihisi wagonjwa kwa sababu hawakupata kile ambacho dini zilizo hai zilikuwa zikiwafundisha na kuwahubiri wafuasi wake."

Sifa ya dini ni kwamba inatilia maanani fitra na maumbile ya mwanadamu ya kuishi na kutokufa na inamhakikishia kwamba hakuna kitu kinachojulikana kama "hakuna au kutokuweko". Na hata kifo ndio daraja pekee linalomtoa mtu kutoka katika ulimwengu huu hadi ulimwengu wa juu na mkubwa zaidi. Kama mnavyojua, kifo ni jambo la kutisha kwa wanadamu na na hata maendeleo makubwa ya kisayansi, hayajaweza kuondokana na jinamizi la mwisho wa maisha ya hapa duniani, yaani kifo.

Hofu ya kifo inarudi kwenye tamaa ya kibinadamu ya kutokufa. Hata wazo la kifo humfanya mtu kuchanganyikiwa na kuwa na wasiwasi. Wale ambao hawauchukulii ukweli wa mtu kuwa si kitu kingine ghairi ya kuwepo kwake kimwili na kuamini kwamba, maisha ya mtu yamejumuishwa katika maisha yake ya kidunia, wanakichukulia kifo kuwa ni maangamizo. Kundi hili linaogopa sana kifo na linafikiri kwamba, njia ya wokovu ni kutokufa katika ulimwengu huu, takwa na tamaa ambayo kamwe haiwezi kutimia.

Moja ya faida za kuvutia za dini ni kwamba inampa mwanadamu nguvu na uwezo unaohitajika wa kudhibiti ghariza na matamanio yake na kudhibiti ipasavyo matamanio yake ya kinafsi. Inapasa kusema kwamba, moja ya mambo ambayo yanatishia jamii ya wanadamu na daima yamesababisha uharibifu mkubwa kwa mataifa mbalimbali ni matamanio yasiyozuiliwa, ubinafsi, choyo, uroho na matamanio ya uasi wa nafsi.

Moja ya kazi chanya za dini ni kwamba, mafundisho yake yanapanda mbegu za matumaini na hali ya kuridhika ndani wa nafsi ya mtu na kuleta matunda ya uhai, harakati na matumaini. Mtu ambaye ana mwelekeo wa kidini huzingatia sheria na mifumo ya ulimwengu kuwa sahihi na ya haki. Ijapokuwa anashuhudia dhulma, umwagaji damu na machafuko duniani, lakini anauona mustakbali wa jamii ya binadamu ukiwa umejaa usalama, haki na mwanga kwa mtazamo chanya. Mtu mwenye imani hutazama ulimwengu kwa matumaini katika hali yoyote ile.

Ayatullah Nasser Makarim Shirazi mwanazuoni na mfasiri wa Qur'ani Tukufu anazungumzia nafasi na mchango wa dini katika kuleta matumaini kwa kusema:

Dini ni tegemeo athirifu  kwa ajili ya kukabiliana na matukio magumu ya maisha na kuzuia athari zisizohitajika za kukata tamaa na kutokuwa na matumaini zinazotokea kwa wanadamu wakati wa kukumbwa na shida za maisha. Mtu mwenye kufungamana na kushikamana na dini, mwenye imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye chanzo cha ujuzi na uwezo usio na mwisho, na kwa kutegemea neema yake, haoni kuwa peke yake na asiye na msaada mbele ya shida yoyote. Akiamini kwamba kila mkanganyiko na tatizo laweza kutatuliwa himaya na msaada wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake wake na hivyo humuepusha na kila mambo yanayokatisha tamaa. Ni kwa sababu hiyo, ndio maana, utapata kuna matukio machache ya watu wa dini ambao katika kutoa radiamali ya matatizo yao huamua kujiua au kukumbwa na magonjwa ya akili ambayo ni matokeo ya kukata tamaa na hisia ya kushindwa maishani.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, basi hadi tutakapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh