Jan 03, 2024 02:45 UTC
  • Jumatano, Januari 3, 2024

Leo ni Jumatano 20 Mfunguo Tisa Jumadithani 1445 Hijria sawa na Januari 3 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1453 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw).

Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu.

Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw).

Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii.

Miaka 125 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alizaliwa huko Khomein Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul-Karim Hairi na Muhammad  Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa.

Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha karibu miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi.

Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu."

Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu."   

Mikhail Gorbachev

Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki. 

Mkombora ya nyuklia

Na miaka 4 iliopita katika siku kama ya leo, Luteni Jenerali Qassem Suleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliuawa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq kwa amri ya moja kwa moja ya Rais Donald Trump wa marekani. Shahidi Qassim Suleimani alizaliwa tarehe 20 Isfand 1335 Hijria Shamsia katika mji wa Kerman.  Wakati wa utoto na kuinukia kwake aliupitisha akiwa pamoja na baba yake. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH alijiunga na kikosi hicho. Wakati wa kuanza vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Qassim Suleimani akawa akitoa mafunzo kwa brigedi za kijeshi mjini Kerman na kuzituma katika medani ya vita. Mwaka 1360 Qassim Suleimani akateuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharallah. Kikosi hicho chini ya uongozi w Qassim Suleimani kilitekeleza operesheni nyingi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu kama Walfajr 8, Karbala 4, Karbala 5 na kadhalika. Mwaka 1389 akateuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa, Kamnada wa Kikosi cha Qusd cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Baada ya kuibuka kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria, Luteni Jenerali Qassim Suleimani alihudhuria katika medani za vita za mataifa hayo akiitikia wito wa viongozi wa nchi hizo na kuwa na nafasi kubwa katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi. Hatimaye aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020 pamoja na Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao wengine wanane katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump.*

Luteni Jenerali Qassem Suleimani

 

Tags