Jan 06, 2024 15:00 UTC
  • Tuujue Uislamu (3)

Assalaamu Alaykum wapenzii wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Kipindi chetu cha Tuujue Uislamu wiki hii ambacho ni sehemu ya tatu ya mfululizo huu kitaaendelea kujadili umuhimu na ulazima wa kuwepo dini kwa wanadamu, na kueleza pia sifa maalumu ya dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu yaani Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

 

Kama tulivyosema, ushahidi na nyaraka za kihistoria zinaonyesha ukweli huu kwamba, katika kipindi chote cha historia hakuna wakati ambao wanadamu hawajawahi kuishi bila dini. Suala la mwanadamu kumili na kuelekea upande wa dini limewafanya wanafikra wengi kutafuta na kudadisi chimbuko lake na kusababisha kuibuka mitazamo tofauti katika suala hili. Kundi lililo na mtazamo wa kukana Mungu yaani walahidi huzingatia mambo kama vile ujahili na ujinga, kutojua mwanadamu mambo yasiyojulikana na hofu yake ya matukio ya kimaumbile kama vile kimbunga, radi na umeme kuwa yenye mchango katika kuibuka dini na wengine wamesisitiza utendaji wa kijamii wa dini.

Lakini uchunguzi wa kina katika uga huuu unawaongoza watu kwenye ukweli kwamba dini daima imekuwa mojawapo ya mahitaji ya kimsingi ya mwanadamu. Qur'ani Tukufu inaichukulia dini kuwa imejengeka kwa mujibu wa fitra na maumbile ya mwanadamu. Kwa kuzingatia kwamba, kushikamana na dini au kuwa mtu wa dini ni muelekeo wa kimaumbile, kuna wakati wanadamu hughafilika na jambo hilo, hivyo Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume waliokuja na risala ili waje kuizindua na kuiamsha fitra hii ya mwanadamu na kumtaka mwanadamu asikilize kwa makini mwito wake wa ndani. Baada ya Mitume wa Allah kuja, kwa amri ya Muumba waliwafundisha wanadamu mafundisho mbalimbali, wakatoa miongozo, sheria, maadili mema n.k ambapo moja ya mafundisho hayo ni kumfanya mwanadamu awe na ufahamu na udiriki sahihi wa maisha. Lengo la mafundisho haya ni kumfanya mwanadamu asijipumbaze tu na maisha ya kila siku na masuala ya kimaada, bali awe upeo wa juu zaidi na kufikia makusudio.

 

 

Kuchomoza nuru ya Uislamu, kuliyafanya mafundisho haya kufikia kiwango chake cha ukamilifu. Kwa hiyo, Uislamu ni dini ya mwisho na kamilifu zaidi. Mafundisho yake ni ya kina, muundo wa mafundisho haya ni kwa namna ambayo, hauwezi kutiwa dosari na ni wa milele. Kwa maana kwamba, madhali mwanadamu angali anaishi duniani, Uislamu ndio ramani ya njia na dira ya sera yake inayoegemea kwenye misingi ya saada na ufanisi. Makusudio ya dini kuwa jumuishi ni kwamba Uislamu haujaacha hata nukta moja katika uwanja wa kutoa mwongozo kwa mwanadamu.

Mwenyezi Mungu anasema katika Surat Nahl Aya ya 89: Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.

Allama Tabatabai, mfasiri mkubwa wa Qur’ani, aandandika katika Tafsir al-Mizan, kuhusu Aya hii: Qur’ani ni kitabu cha mwongozo kwa umma kwa ujumla, na maana ya kila kitu katika Aya hii ni yale mambo yote ambayo yanahusiana na kutoa mwongozo kwa mwanadamu. Elimu yote inayohusiana na asili na ufufuo, maadili mema, simulizi, mawaidha na nasaha ambazo watu wanahitaji kwa ajili ya kupata wongofu.

Yote haya yameelezwa na kubainishwa ndani ya Quran. Imekuja katika Tafsir Nemooneh ya Ayatullah Makarim Shirazi katika kubainisha Aya hii ya kwamba, neno kila kitu katika Aya hii linamaanisha mambo yote ambayo ni ya lazima kwa ajili ya ukamilifu wa pande zote kwa ajili ya mtu binafsi na jamii, siyo kwa maana kwamba Qur’ani ni tabu kubwa la maarifa yaani Ensaiklopidia ambayo ina maelezo yote ya elimu ya hisabati, jiografia, kemia na fizikia ndani yake. Kwa hiyo, Qur'an ni kitabu chenye nuru na mwongozo, na kwa mafundisho yake ya milele, inachukuliwa kuwa katiba ya maisha ya watu wanaomjua Mwenyezi Mungu. Imamu Ali bin Mussa al-Ridha (a.s.) anasema kuhusu kuwa jumuishi kitabu cha mwisho cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani kama alivyonukuliwa katika kitabu cha Uyun Akhbar al-Ridha kwamba: Mungu hakuifanya Qur'ani kuwa kwa ajili ya muda na watu maalumu. Qur'an ni mpya kwa nyakati zote na kwa watu wote mpaka siku ya Kiyama.

 

 

Inafahamika kwa uwazi kabisa kutoka katika mkusanyiko wa mafundisho na mipango ya Uislamu kwamba, msingi wa Uislamu umejengeka juu ya kutafakari na kutumia akili. Hii ni sifa maalumu ya Uislamu. Na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kutafakari katika Uislamu kwa ajili ya kufikia ustawi wa kielimu na maarifa kuna nafasi na daraja maalumu. Kutafakari kunamaanisha kutumia nguvu na uwezo wa akili kufikiri kwa ajili ya kutoa na kuleta mambo yenye manufaa na yenye kujenga. Akili ni moja ya zawadi na tunu kuu za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu ambayo kwa msaada wake mwanadamu anaweza kufikia saada na ufanisi. Mtume (saww) amenukuliwa akisema:

Mwenyezi Mungu hajawapatia waja wake kitu bora zaidi kuliko akili. Lakini ni lazima kusemwa kwamba wengi miongoni mwa viongozi wa dini na wahubiri wa dini za kabla ya Uislamu, waliiona dini kuwa ni hakika na ukweli ambao unakinzana na akili, hasa katika ufahamu wa kanisa wa mafundisho ya Yesu Kikristo. Waliamini kwamba dini ni jambo la Kimungu na mwanadamu haruhusiwi kuifikiria. Lakini Uislamu siyo tu kwamba, haukupingana na akili na kutafakari, bali pia ulitafuta msaada kutoka kwake kwa njia mbalimbali na ukaitegemea pakubwa.  Kutumia akili na kutafakari katika Uislamu kuna nafasi muhimu kwa namna ambayo hata Usul Dini yaani Misingi ya Dini ambayo, Tawhidi, yaani kumpwekesha Mwenyezi Mungu, al-Nubuwa yaani Utume, al-Maad yenye maana Ufufuo nayo ni kuamini kwamba mwanadamu baada ya kifo atafufuliwa Siku ya Kiyama na kulipwa kutokana na matendo yake mema au mabaya, Uadilifu ambayo ni kuamini kwamba, Mwenyezi Mungu ni muadilifu na hamdhulumu yeyote na msingi wa mwisho ni Uimamu. Ni wajibu kwa kila Mwislamu kujifunza na kuitambua misingi hii haijuzu kukalidi na kufuata katika haya. Uislamu umemfungulia njia mbele yake mwanadamu kwa ajili ya kufahamu njia ambayo ni akili na kutafakari na unasisitiza kwamba, mwanadamu anapaswa kufanya uchunguzi na utafuti kwa uhuru kamili kuhusiana na Usul al-Din yaani Misingi ya Dini ya Uislamu.

 

Na hadi hapa ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya Tuujue Uislamu. Wassalaam Aalaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.