Nigeria yapinga vikali vitisho vya Trump, yasema mamlaka yake ya kujitawala hayajadiliwi
-
Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria
Serikali ya Nigeria imepinga vikali uingiliaji wowote wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo ikisisitiza kwamba "mamlaka ya kitaifa hayawezi kujadiliwa," na kwamba inachunguza matukio ya hivi karibuni na kuwafuatilia wale wote waliohusika.
Taarifa hiyo ya serikali ya Nigeria imetolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia kwamba atafanya mashambulizi ndani ya Nigeria kujibu kile alichodai ni "mauaji ya kutisha ya Wakristo," kufuatia ripoti za kuuawa raia kadhaa katika mashambulizi yanayohusishwa na makundi ya waasi huko kaskazini mwa Nigeria.
Serikali ya Nigeria imeahidi kuendeleza juhudi za kupambana na itikadi kali, ikielezea matumaini kwamba Marekani itaendelea kuwa mshirika wa karibu.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesema "Serikali ya Shirikisho itaendelea kuwalinda raia wote, bila kujali mbari, imani au dini zao.
Mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotokea katika Jimbo la Plateau, yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 30 katika vijiji vyenye waumini wengi wa Kikristo na yamehusishwa na wanamgambo wanaoaminika kuwa na uhusiano na makundi yenye msimamo mkali.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba matamshi ya Trump yana mwelekeo wa siasa za uchaguzi wa ndani, kwa sababu anataka kuimarisha uungwaji mkono wa wananchi kutoka kwa kambi ya kiinjili ya wahafidhina.
Wataalamu pia wanasema madai kwamba kinachotokea Nigeria ni "mauaji ya kimbari ya Wakristo" ni uwongo na hayana mashiko.
Wamesisitiza kuwa hujuma na mashambulio yanayofanywa na makundi yanayobeba silaha ndani ya Nigeria yanawalenga Wakristo, Waislamu na hata wafuasi wa dini za jadi.
Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kujizuia na kuzitaka pande zote kuheshimu sheria za kimataifa na kutochukua hatua za upande mmoja ambazo zinaweza kuyumbisha amani ya eneo hilo.
UN pia imetaka kufanyike uchunguzi huru kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Nigeria na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.