Jan 06, 2024 15:00 UTC
  • Tuujue Uislamu (4)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu ambacho hukujieni kila juma siku na wakati kama huu.

Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 4 ya mfulilizo huu kitazungumzia sifa zingine maalumu za dini ya Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. 

Moja ya sifa muhimu za dini ya Uislamu ni kuwa, dini hii inaendana kikamilifu na fitra na maumbile ya mwanadamu. Kwa msingi huo, mafundisho yake yanajumuisha engo na pande zote za uwepo wa mwanadamu na yanadhamini ukuaji na kuchanua kwa vipaji vyake kuelekea saada na ukamilifu. Kwa kutegemea Aya za Qur’ani, inawezekana kufahamika kwamba, mwanadamu ameumbwa akiwa na engo na pande mbili ambazo ni mwili na roho. Kwa upande mmoja, kuna mvuto na motisha ndani yake zinazompeleka kukidhi matamanio na mahitaji ya kimaada; na zaidi ya hayo, mwanadamu ana vipaji na uwezo unaomshajiisha kuelekea upande wa haki, umaanawi na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Uislamu ikiwa dini kamilifu zaidi mongoni mwa dini za mbinguni, una mipango na mikakati inayoendana na mahitaji ya mwadamu na muelekeo wa kifitra na kimaumbile. Muelekeo wa kifitra na kimaumbile ni wa aina moja na kwa muktadha huo wanadamu hao mtaji wao ni mmoja yaani fitra na maumbile.

Sifa nyingine ya Uislamu ni kuwa, dini hii ya Mwenyezi Mungu, ni dini ya ulimwengu wote na ya zama zote. Uislamu haukomei kwenye eneo maalumu la kijiografia. Wakati wa Utume wake, Mtume wa Uislamu (saww) aliwaandikia barua viongozi na  wafalme wa Roma, Iran, Misri na kadhalika na kuwalingania waukubali Uislamu. Kama Uislamu usingekuwa dini ya ulimwengu wote, mwaliko na ulinganiaji huo haungetolewa.

 

 

Aya za Qur'ani zinaichukulia dini ya Kiislamu kuwa ni mwongozo wa watu wote. Mwenyezi Mungu anasema katika Sura Swaad Aya ya 87:

Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.

Katika Aya hii, imesisitizwa kuwa Qur'an imeshushwa na Mtume ametumwa kwa ajili ya walimwengu wote. Katika Aya nyingine, Mwenyezi Mungu anatoa habari ya ushindi wa dini ya Kiislamu juu ya dini zote, na katika Sura At-Tawbah, Aya ya 33 anasema:

Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapokuwa washirikina watachukia.

Kwa mujibu wa sifa hizi, inaweza kusemwa kuwa, tofauti na dini nyingine za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa kwa nyakati maalum na kwa watu maalumu, Uislamu ni dini ya wanadamu wote kwa nyakati tofauti. Sifa hii maalumu ya Uislamu pia inahusiana na sifa za mafundisho yake.

Kwa ibara nyingine ya wazi na nyepesi zaidi, inaweza kusemwa kwamba, mafundisho ya Kiislamu yamewasilishwa katika muundo jumla. Yaani, Uislamu umewasilisha kile ambacho ni cha lazima kwa ajili ya saada na ufanisi wa mwanadamu katika mfumo wa sheria za jumla, na bila shaka unabainisha kwamba sheria hizi za jumla zinapaswa kutumika kwa mambo madogo katika hali tofauti za wakati na mahali.

Mintarafu hiyo, mafundisho ya dini ya Kiislamu yanakwenda sambamba na  wakati na hali tofauti za mahali na tamaduni tofauti. Kwa utaratibu huu wa Uislamu, hakuna haja ya dini mpya kuja na Uislamu ni dini ya mwisho ya mbinguni iliyoteremshwa kwa wanadamu.

Miongoni mwa sifa zingine za Uislamu, ni kwamba, dini hii ni kamili na jumuishi. Kuwa jumuishi na kamili dini ya Kiislamu ni mambo mawili ambayo yana uhusiano.

 

Kundi la wanafikra wa Kiislamu wanaona kwamba, kuwa jumuishi dini  ndio ile ile hali jumuishi ya Qur'an na ili kubainisha kwamba, Qur'an ni jumuishi wametegemea Aya za Qur'an kama hoja ya hilo. Kwa mfano katika Aya ya 89 ya Surah Nahl Mwenyezi Mungu anasema:

Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika kila umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.

Makusudio ya kila kitu katika Aya hii ni mambo yote ambayo ni ya lazima kwa ajili ya ukamilifu wa pande zote kwa ajili ya mtu binafsi na jamii.

 

Sifa nyingine ya Uislamu inayoonyesha ukamilifu wake ni kuzingatia anthropolojia yaani elimu ya kumtambua mwanadamu. Dini jumuishi inapaswa kuwa na utambuzi wa kina wa kumjua wanadamu. Katika dini hii, nafasi ya mwanadamu katika ulimwengu, visababishi vya kufikia ukamilifu mwanadamu, mahitaji ya mwanadamu na njia za kukidhi, uhusiano wa mwanadamu na yeye mwenyewe, na Mwenyezi Mungu, maumbile na wengine na mipango Kimwenyezi Mungu inayotawala kwa maisha ya mtu binafsi na jamii, yote hayo yamebainishwa. Urahisi na usahali wa mafundisho ya Kiislamu ni moja ya sifa bainifu za dini hii. Sifa hii nayo ni muhimu.

Baadhi ya watu huuliza jinsi dini iliyoteremshwa zamani inaweza vipi kukidhi mahitaji ya watu katika hali tofauti za nyakati? Au sheria za Uislamu, ambazo ziliteremshwa karne kumi na nne zilizopita na Mwenyezi Mungu ili kuongoza na kusimamia maisha ya mwanadamu, zinawezaje kujitabikisha na mahitaji ya wakati huu na kujibu mahitaji mbalimbali ya watu katika zama hizi?

Ili kujibu swali hili, kwanza kabisa, tunahitaji kueleza aina za mahitaji ya binadamu. Mahitaji ya mwanadamu yamegawanyika katika makundi mawili. Mahitaji ya awali na ya kimsingi na mahitaji ya daraja la pili. Mahitaji ya msingi ni mahitaji ambayo yana chimbuko na mzizi wa masuala ya matamanio na ya kimaumbile, na madhali mwanadamu huyu angali hai bila kuzingatia zama na sehemu, ni mahitaji ya daima na milele kwake, ni kama vile mahitahji chakula, mavazi na makazi; au mahitaji ya kiroho kama vile kuhitajia kuabudu, hitajio la kufahamu na kujua au mahitaji ya kijamii  kama kushirikiana na wengine, kuwa na uhuru n.k.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Tuujue Uislamu umefikia ukingoni. Tukutane tena juma lijalo.