Feb 13, 2024 04:47 UTC
  • Tuujue Uislamu (6)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 Katika sehemu ya 6 ya mfululizo huu juma hili, tutazungumzia kujali suala la kumtambua Muumba na Tawhidi yaani kumpwekesha Mwenyezi Mungu ukiwa msingi muhimu kabisa wa kiitikadi wa Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Wanafikra wote, wawe ni wale wenye mielekeo ya kimaada au wenye itikadi juu ya kuweko Muumba, wanakubaliana juu ya ukweli kwamba dunia ina sababu ya kwanza, na uwepo wake unatokana na yenyewe mwenyewe. Lakini wanafalsafa wa kimaada huona kisababishi cha kwanza kuwa ni maada na wanafalsafa wa Kimungu wanaona sababu ya kwanza kuwa ni Mungu. Kuwepo kwa sababu ya kwanza au sababu ya milele ni kwa sababu mlolongo wa sababu na athari hauwezi kuendelea bila kikomo na kisha tukafikia uwepo ambao wenyewe ndio sababu kuu na sio athari ya kitu kingine chochote. Ina maana kwamba nafsi yake imetokana na yeye mwenyewe na kwa kawaida imekuwa na itakuwa hivyo.

Katika falsafa, mjadala na maudhui hii inajulikana kama "ubatilifu wa mlolongo"; kwa maana kwamba, haiwezekani kwa mlolongo wa sababu uendelee kwa muda usiojulikana na bila ya kikomo. Sababu ya ubatilifu wake pia iko wazi, kwa sababu kila athari ni lazima iwe na kisababishi na mhitaji, na bila ya kuweko kisababishi yenyewe, si chochote si lolote. Kwa maana kwamba, uwepo wake unategemea kisababishi chake. Sasa tukija katika suala la muumba na viumbe au dunia na aliyeiumba tunakuta kwamba, ni vivyo hivyo, kwa maana kwamba, ulimwengu lazima uwe na aliyeuumba na bila yeye si lolote si chochote, kama ambavyo kwa mwanadamu pia ni hivyo hivyo.

Ili kumjua Mwenyezi Mungu, kuna njia mbalimbali ambazo zimetajwa katika maandiko na vyanzo vya kidini na vyanzo na maandishi yanayohusiana na mada za kiitikadi. Baadhi ya watu wanamjua Mungu wao kwa njia rahisi sana na kumtumikia. Lakini wanadamu wengine pia wanakabiliwa na mashaka mengi na lazima wafikie hatima na makusudio yao kupitia njia zenye hoja na misingi thabiti. Hata hivyo, wanadamu wote wana kitu kimoja sawa, nacho ni kwamba, kimaumbile wanamjua Mwenyezi Mungu na wana hali ya mwelekeo kuelekea jambo hilo.

 

Suala la dhati na maumbile ya mwanadamu kumuelekea Mungu limejitokeza kwa namna mbalimbali katika historia na limeambatana na hali ya panda na shuka. Ingawa wakati mwingine utambuzi huu umekumbwa na hali ya mghafala au kukengeuka, lakini mwelekeo kuelekea Mungu haujawahi kuzimwa katika dhati na maumbile ya mwanadamu. Watu wanaomtafuta Mungu wanaweza kulinganishwa na watu wenye kiu wanaotafuta maji katika jangwa kavu na lenye jua kali ili kukata kiu yao. 

Wanapofika kwenye chemchemi na kupata maji safi na matamu, hujihisi kuwa na furaha isiyo na kifani. Wale ambao, baada ya kutafuta sana, hufikia natija juu ya kuwepo kwa Muumba mwenye busara na mbunifu wa kuwepo, wana hisia sawa na wale waliofanikiwa kupata chemchemi ya maji matamu baada ya kutangatanga na kuhangaika jangwani.

Yumkini njia ya kwanza na ambayo ni nyepesi ya kumtambua Mwenyezi Mungu ni kusoma na kufanya uchunguzi kuhusiana na mfumo wa ulimwengu na vilivyomo.

Kwa maana kwamba, tunapaswa kuangalia viumbe mbalimbali na vitu tofauti vilivyoko katika ulimwengu na kuona kama kuna ishara ya Muumba katika viumbe au la? Njia ya kumjua Mwenyezi Mungu ni kutafakari juu ya ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu na, kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, kutafakari juu ya Aya yaani ishara za Mwenyezi Mungu. Ni kana kwamba kila moja ya matukio ya ulimwengu ardhini na angani na kwa wanadamu yana ishara ya Mungu anayefahamika nao na kuelekeza moyo kwenye kitovu cha uwepo ambacho kipo kila wakati na kila mahali.

 

Mpangilio na nidhamu madhubuti ya ulimwengu huu, kuchomoza jua na kuzama kwake kwa mpangilio maalumu zote hizi ni ishara za kuweko muendeshaji na msimamizi wa haya ambaye si mwingine bali ni Mwenyezi Mungu.

Popote kunaposhuhudiwa nidhamu na mpangilio maalumu bila shaka hilo linaonyesha kuwepo kwa mpangiliaji na muendeshaji wa hilo. Kulingana na maoni ya wanasayansi, kuna utaratibu wa kushangaza na wa kimuujiza katika viumbe vyote vya ulimwengu.

Katika mwili huu wa mwanadamu, kazi za kushangaza zaidi zilizo na mpangilio wa busara zinaweza kuonekana. Wacha tufikirie kidogo juu ya muundo wa uwepo wa mwanadamu. Vipengele vya mwili wa mwanadamu vinatambuliwa mara kwa mara na kulingana na mpango wa kina, na kila kimoja huwekwa mahali pake. Kila seli ya mwili ni mfumo wenye malengo kusudiwa, mzunguko wa damu, mapigo ya moyo, pumzi, kuota nywele, kucha, machozi, mate, na vinginevyo ambapo kila kimoja hutoka kwa wakati maalumu na kwa sababu maalumu. Kwa mfano huzuni na masikitiko hupelekea kutokwa na machozi na sio kutokwa na kingine kama mate n.k

Mifano hii na mingineyo inaonyesha kuweko nidhamu na mpangilio usio na mithili wa dunia hii na viumbe vyake jambo linaloonyesha kuwa kuna muumba na msimamizi wa haya. Mifano hii iko mingi. Mfano mwingine na uratibu wa ajabu uliopo baina ya kutoka maziwa katika nyonyo ya mama na kuzaliwa mtoto jambo ambalo hutokea kwa pamoja. Aidha tukitupia jicho maisha ya nyuki na asali. Nyuki hutoka kila asubuhi katika mizinga na baada ya kukata masafa marefu wakitua na kufyonza maua mbalimbali yenye uturi, inapofikia jioni hurejea katika mizinga yao bila ya kupotea njia.

Hapana shaka kuwa, kadiri wigo wa elimu na maarifa ya mwanadamu unavyokuwa mpana zaidi ndio pazia zinavyoondoka mbele yake na kudhihirika hekima zaidi za uumbaji. Mifano hii na mingineyo inaonyesha na kuthibitisha kwamba, ulimwengu huu una Muumba ambaye ni mjuzi mwenye uwezo na mwenye nidhamu na mpangalio wa hali ya juu.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umemalizika, hivyo sina buudi kukomea hapa nikitaraji kuwa amtanjiunga nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Tuujue Uislamu.

Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.