Mar 01, 2024 08:04 UTC
  • Tuujue Uislamu (7)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Tulisema katika kipindi chetu cha juma lililopita kwamba: Tunapaswa kuangalia viumbe mbalimbali na vitu tofauti vilivyoko katika ulimwengu na kuona kama kuna ishara ya Muumba katika viumbe au la? Njia ya kumjua Mwenyezi Mungu ni kutafakari juu ya ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu na, kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, kutafakari juu ya Aya yaani ishara za Mwenyezi Mungu. Karibuni kutegea sikio  sehemu ya 7 ya mfululizo huu juma hili.

 

Ni jambo lisilo na shaka kuwa, ili kudiriki uhakika wa ulimwengu huu na vilivyomo, kadiri wigo wa tafakuri unavyokuwa mpana na kadiri tunavyofanya uhakiki na utafiti zaidi kuhusiana na matukio mbalimbali ya ulimwengu huu bado hatutakuwa na nyenzo za kutosha za kuweza kufikia siri zote za ulimwengu huu. Kwa mtazamo huu, ulimwengu unagawanyika katika sehemu kuu mbili: Dhahiri na kificho au yanayoonekana na yasiyoonekana.

Ni ukweli usiokanushika ya kwamba uwepo hauwezi kujumlishwa katika masuala ya hisi na kuhisi ambayo ni katika uwanja wa elimu ya majaribio na kwa maneno mengine ni kuwa, ukweli mwingi hauwezi kueleweka kwa hisi zetu za nje au aina za utambuzi kama zinavyojulikana pia yaani kuona, kusikia, kunusa na kadhalika.

Kuelewa siri za uumbaji kunahitaji zana nyingine na wakati huo huo inategemea kwa kiasi fulani juu ya uwezo wetu wa mawazo, weledi na ufahamu. Hapana shaka kuwa, kila ambavyo akili na tafakuri inavyokuja na kusaidia tajiriba na hisi za binadamu, basi ni vivyo hivyo ambavyo itawezekana kujua mambo mengi ya hakika na ya ukweli.

Katika za Mtume (saw) na Ahlul-Bayt zake (as) akili inafananishwa na nuru ambayo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu. Akili humsaidia mwanadamu kutofautisha haki na batili na kheri na shari. Ali (a.s.) anasema kuhusiana na hili: Imani ya kuwepo kwa Mungu inapatikana kupitia akili, na kwa kukiri kuwepo kwa Mungu, imani inakamilika.

Tukichunguza kitabu cha uumbaji, tutaona kwamba hekima na mipango ya hali ya juu ilichangia kuumba ulimwengu huu mkubwa. Huu ni uthibitisho rahisi na wa wazi. Kulingana na hoja hii, mpangilio wowote wenye lengo ni ishara ya mpangaji mwenye akili, huku ulimwengu ukiwa umejaa dalili za utaratibu na mipango.

 

Ulimwengu wa uwepo, wenyewe ndio uthibitisho wa wazi zaidi wa kumtambua Mwenyezi Mungu. Quran imewaita na kuwataka watu kusoma kitabu cha uumbaji kwa msisitizo mwingi. Qur’ani haikutosheka na hili bali imefungua njia kwa wanadamu kusoma na kuchunguza kwa kutoa mifano ya matukio ya ajabu ya dunia.

Kwa ajili hiyo, Qur’ani imewaalika wanadamu kufikiria ulimwengu wa uumbaji, ili kila mmoja aweze kuelewa mifano ya wazi ya utaratibu wa ulimwengu kwa kutumia elimu na kipaji chake. Kulingana na nidhamu na mpangilio wa kustaajabisha unaoweza kuonekana katika kila chembe ya ulimwengu, kila mwanadamu anaweza kutambua kuwepo kwa mpangiliaji na msimamizi mwenye ufahamu ambaye amelifanya hilo kwa hekima na busara.

Kama tulivyoashiria katika kipindi kilichotangulia ni kuwa, mpangilio na nidhamu madhubuti ya ulimwengu huu, kuchomoza jua na kuzama kwake kwa mpangilio maalumu zote hizi ni ishara za kuweko muendeshaji na msimamizi wa haya ambaye si mwingine bali ni Mwenyezi Mungu.

Popote kunaposhuhudiwa nidhamu na mpangilio maalumu bila shaka hilo linaonyesha kuwepo kwa mpangiliaji na muendeshaji wa hilo. Kulingana na maoni ya wanasayansi, kuna utaratibu wa kushangaza na wa kimuujiza katika viumbe vyote vya ulimwengu.

Siri, mifumo na mipangilio imara ya ulimwengu wa uumbaji ni kama bahari ya kina na pwani zisizoonekana. Mwanadamu kwa elimu yake ya sasa amepiga  hatua chache tu ndogo, na kadiri anavyosonga mbele katika upande wa elimu na maarifa, ndivyo mshangao wake mkubwa juu ya adhama ya uwepo unavyozidi kuongezeka na hivyo kupanua mipaka ya ujuzi wake.

 

Mwanafizikia mmoja anasema: Kadiri nilivyozidi kusoma na kutazama kila kitu kuanzia atomu hadi kundi la nyota, kutoka kwa vijidudu maradhi hadi wanadamu, niligundua kwamba, pamoja na kuongezeka kwa ujuzi wangu, upeo wa mambo yangu yasiyojulikana umepanuka siku baada ya siku. Kwa maana kwamba, upeo wa ujinga wangu na yale nisiyoyafahamu ulizidi kupanuka.

Maneno kama haya, ambayo mara nyingi husikika kati ya wanafikra, yanaonyesha kuwa wanadamu hawajapiga zaidi ya hatua chache kwenye ngazi ya juu ya elimu na maarifa. Kwa hivyo, wakati Einstein, mwanasayansi maarufu na mwanafizikia mtajika, alipotakiwa kubainisha uwiano ujuzi na anayoyajua mkabala wa yale aliyoyafahamu, alijibu kama ifuatavyo akiwa amesimama karibu na ngazi ya maktaba yake: Uwiano wa mawili haya kwa kila moja, ni kama uwiano wa ngazi hii kwa nafasi isiyo na kikomo ya mbingu na bado sijapanda ngazi ya elimu ghairi ya hatua chache kwenye ngazi ya elimu.

Pamoja na hayo, ni sehemu tu ya ujuzi wa sasa wa mwanadamu kuhusu adhama ya uumbaji ambayo inatosha kumtambua kuwa ni Muumba mwenye hekima, busara na nguvu, na inathibitisha wazi kwamba mpangilio sahihi na tata kama huo, kwa vyovyote vile, bila ya kuwepo kwa chanzo kikubwa chenye nguvu ni jambo ambalo haliwezekani. Mfumo wa dunia na mpangilio wake makini kwa hakika ni ithbati tosha ya kuweko muumba mwenye nguvu.

Tunakamilisha kipindi chetu juma hili kwa kunukuu baadhi ya Aya za Qur'ani Tukufu:

Mwenyezi Mungu anasema katika Surat at-Tawba Aya ya 116 kwamba:

Hakika Mwenyezi Mungu ni mmiliki wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, Hana mshirika katika uumbaji, uendeshaji, ustahiki wa kuabudiwa na uwekaji sheria. Anampa uhai Anayemtaka na anamfisha Anayemtaka. Na hakuna yoyote, isipokuwa Mwenyezi Mungu, wa kuyasimamia mambo yenu wala wa kuwapa ushindi juu ya adui wenu.

Aidha Aya ya 126 ya Surat Nisaa inasema:

Ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuvizunguka vitu vyote.

 

Na hadi hapa ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili. Tukutane tebna wiki ijayo katika sehemu nyingine ya nmfululizo huu. Wassalaam alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh