Jun 06, 2024 04:25 UTC
  • Alkhamisi, 6 Juni, 2024

Leo ni Alkhamisi 28 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria sawa na 6 Juni 2024 Miladia.

Tarehe 28 Dhilqaada miaka 1085 iliyopita mwanazuoni wa Kiislamu, Abul Qasim Tabarani, alifariki dunia katika mji wa kihistoria wa Isfahan nchini Iran. Tabarani alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Hadithi wa karne ya nne Hijria na alifanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya Hadithi za Mtume Muuhammad (saw). Alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi baada ya utafiti na uchunguzi wa miaka 33. Tabarani ameandika vitabu vikubwa vitatu vya Hadithi kwa majina ya Al Muujamul Kabiir", al Muujamul Wasiit na al Muujamus Swaghir. ***

 

Katika siku kama ya leo, miaka 225 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru. ***

Alexander Pushkin

 

Miaka 42 iliyopita katika siku kkama ya leo, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Lebanon. Katika uvamizi huo, jeshi la Israel liliuvamia na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bairut. Aidha askari hao wa utawala haramu wa Kizayuni, waliharibu miundombinu, viwanda na viunga vya mji huo, sanjari na kutekeleza jinai mbalimbali dhidi ya wakazi wake. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa Wazayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mwezi Septemba mwaka huo huo, jeshi hilo likatekeleza mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika kambi mbili za sabra nashatila karibu na mji mkuu wa Lebanona, Bairut. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 2000, kufuatia ushindi wa wanamapamgano wa Hizbullah, wanajeshi vamizi wa Israel walilazimika kuondoka kwa madhila katika maeneo yote ya Lebanon waliyokuwa wameyakalia kwa mabavu. ***

 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Juni 1984, jeshi la India lilishambulia hekalu kubwa la Masingasinga lililojulikana kama Hekalu la Dhahabu katika mjini wa Amritsar makao makuu ya jimbo la Punjab, magharibi mwa India na kuua waasi wa Kisingasinga wasiopungua 1,000. Serikali ya India ilidai kuwa shambulio hilo lilifanywa baada ya kupatikana habari za kufichwa silaha nyingi kwenye hekalu hilo, kwa shabaha ya kuanzisha uasi na mashambulizi dhidi ya serikali kuu. Masingasinga hao nao walilipiza kisasi kwa kumuuwa Indira Ghandi, Waziri Mkuu wa India mwaka huohuo, kiongozi ambaye ndiye aliyetoa amri ya kushambuliwa hekalu hilo. ***

 

Na tarehe 6 Juni ni Siku Taifa ya Sweden. Falsafa ya kupewa siku hii jina hilo la Siku ya Taifa ya Sweden ni tukio la kutungwa katiba ya kwanza ya nchi hiyo miaka 206 iliyopita katika siku kama ya leo. Sweden ni nchi yenye ukubwa wa kilomitamraba 449,964; iko kaskazini ya Ulaya kando ya Bahari ya Baltik na imepakana na nchi za Norway, Finland na Denmark. Nchi hiyo ina idadi ya watu milioni tisa ambao karibu asilimia 90 miongoni mwao wana asili ya Sweden na wanafuata madhehebu ya Protestanti. Lugha ya taifa nchi hiyo ni Kisweden na mji mkuu wake ni Stockholm. Mfumo wa kisiasa wa Sweden ni Ufalme wa Kikatiba ambapo cheo cha ufalme ni cha heshima tu. Sweden inatambuliwa kuwa moja ya nchi tajiri zaidi na zilizoendelea zaidi duniani. ***